Ngao ya Jamii 2024, makipa ndio wataamua
MECHI za msimu huu za Ngao ya Jamii zina msisimko wake kwani timu hizo zinakutana zikiwa na sura mpya, lakini cha kuzingatia ni kwamba zote zinaongozwa na makipa wa kigeni, hivyo wao ndio watakaoamua timu zao ziende fainali ama kucheza mechi za mshindi wa tatu kutokana na rekodi zao. Endelea nayo...
Djigui Diarra (Yanga)
Hakuna shaka juu ya uwezo wa Diarra anapokuwa langoni kwani tangu ajiunge na timu hiyo amekuwa kipa namba moja akiwatoa Ramadhani Kabwili, Metacha Mnata, Farouk Shikhalo na wengine waliopita kikosini hapo.
Diarra alisajiliwa na Yanga Agosti 2021 akitokea Stade Malien ya nchini kwao Mali na tayari amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kusalia kikosini hapo hadi msimu wa 2026-27.
Yanga msimu huu imeongeza kipa mmoja mzawa, Khomeiny Abubakar kutoka Ihefu na kumuongezea mkataba Aboutwalib Mshery kuendelea na klabu hiyo.
Ukiangalia rekodi za Diarra zinawafunika makipa wote wawili kwani hadi sasa mwenye uhakika wa namba eneo hilo ni yeye kutokana na kiwango alichoonyesha ndani ya misimu mitatu Jangwani.
Diarra sio mgeni wa mechi za Dabi akicheza mechi 10 dhidi ya Wekundu wa Msimbazi tangu aanze kuitumikia timu hiyo.
Dabi yake ya kwanza kucheza dhidi ya Simba ilikuwa Septemba 25, 2021 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na akapata ushindi wake wa kwanza kwa bao la mshambuliaji, Fiston Mayele.
Hadi sasa kipa huyo amecheza mechi 10 za Dabi ya Kariakoo ambapo sita ni za ligi akishinda mbili zote za msimu uliopita 5-1 na 2-1 akipoteza moja na sare tatu.
Nje ya hapo amecheza Dabi za Kariakoo tatu za Ngao ya Jamii akishinda mbili na kupoteza moja ya msimu uliopita kwa penalti iliyopigwa Tanga, lakini pia akikutana na Wekundu mara moja katika Kombe la FA akipata ushindi.
Kwa ujumla ameitumikia Yanga dakika 900 akiruhusu mabao sita pekee ndani ya mechi hizo.
Tangu amefika Tanzania kwenye kabati la tuzo ameibuka kipa bora wa msimu mara tatu mfululizo (mbili katika ligi na moja Shirikisho) na ameisaidia timu hiyo kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara mfululizo na mataji mawili ya Kombe la Shirikisho (FA) amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza.
Moussa Camara (Simba)
Simba hadi sasa ina makipa watano -- watatu wazawa, Ally Salim, Aishi Manula na Hussein Abel na wawili wa kigeni, Ayoub Lakred na Moussa Camara.
Makipa wote wanne wamecheza mechi mbalimbali za mashindano isipokuwa Camara ambaye amesajiliwa hivi karibuni akitokea Horoya AC ya Guinea akicheza kwenye mechi ya kirafiki Simba Day dhidi ya APR ya Rwanda.
Baada ya Manula ambaye ndio alikuwa kipa tegemeo kwenye kikosi cha Simba kuumia na kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita, timu hiyo iliingia sokoni na kumsajili Lakred ambaye alionekana kuziba pengo la ‘Tanzania One’ Manula.
Baada ya kuziba pengo vizuri, Lakred akawa kipa tegemeo. Lakini baada ya naye kuumia atakaa nje ya uwanja kwa muda, ndipo ikamsajili Camara kuwa mbadala wake.
Lakred tangu ametua Tanzania amecheza dabi moja msimu uliopita akipoteza kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Aziz KI na Joseph Guede ambaye ametimkia Singida Black Stars.
Hadi sasa Simba katika Dabi bado haijajulikana ni kipa gani anaweza kusimama langoni kutokana na watatu wazoefu kuumia, Salim, Manula na Lakred.
Kama Salim atakuwa vizuri Simba inaweza kumpa nafasi kutokana na uzoefu alionao na ana rekodi yake ya kipekee akiwa hajawahi kuruhusu bao kwenye mechi mbili dhidi ya Yanga ambazo amewahi kuiongoza Simba, lakini pia akiwa ndiye shujaa wa Wekundu walipochukua taji pekee wanaloshikilia msimu uliopita la Ngao ya Jamii alipodaka penalti za Yanga jijini Tanga.
Katika dabi ya mwisho ya msimu 2022/23 kwa Simba langoni alisimama Salim na Wekundu kushinda kwa mabao 2-0 mabao yaliyofungwa na Kibu Denis na Henock Inonga.
Kwa rekodi hiyo ni wazi Salim ana nafasi kubwa ya kusimama langoni kuiongoza Simba.
Mohammed
Mustafa (Azam FC)
Msimu wa 2022/23 na mwanzoni mwa msimu uliopita wa 2023/24 havikuwa vipindi vizuri kwa makipa wa Azam FC ambao walipata majeraha.
Majeraha hayo yaliwafanya Azam FC kumuomba Mohamed Mustafa kwa mkopo akitokea Al Merreikh ya Sudan.
Mustafa alijiunga na Azam katika dirisha dogo la msimu uliopita na amekuwa nguzo imara ya mafanikio ya Wanalambalamba iliyokata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 20 na kuwafanya mabosi wa timu hiyo kufanya mchakato wa kumnunua moja kwa moja.
Mustafa amekuwa muhimili mkubwa ndani ya timu hiyo ambapo amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza ambacho amekiwezesha kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara na kufuzu Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Ndani ya michezo 30 ya Ligi Kuu ameruhusu mabao 21 pekee ikiwa ni kati ya timu zilizofungwa mabao machache.
Ley Matampi (Coastal Union)
Hivi karibuni kwenye usiku wa tuzo za TFF aliondoka na ile ya kipa bora wa Ligi Kuu akiwashinda Diarra wa Yanga na Lakred wa Simba.
Ndio kipa aliyeruhusu mabao machache baada ya Diarra wa Yanga aliyefungwa 14 na Matampi akiruhusu 19. Ni mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho na anaweza kuamua matokeo vs Azam leo.