Napoli kubadili jina kumuenzi Diego Maradona

Muktasari:

Napoli inapanga kubadili jina la uwanja wao kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Diego Maradona aliyefariki juzi usiku akiwa na miaka 60.

Naples, Italia. Napoli inapanga kubadili jina la uwanja wao kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Diego Maradona aliyefariki juzi usiku akiwa na miaka 60.

Mchezaji huyo wa zamani wa Argentine alipata mshituko wa moyo akiwa nyumbani Jumatano ikiwa ni iwki mbili tangu alipotoka hospitali alikofanyiwa upasuaji wa kichwa kutoa damu iliyodondoka kwenye ubongo.

Maradona anakumbukwa zaidi kwa kuiongoza Argentina kwenye fainali tatu za Kombe la Dunia, akicheza kwa mafanikio na mchango mkubwa kwenye fainali za 1986.

Lakini katika ngazi ya klabu, alikuwa na maisha mazuri alipoichezea Napoli kati ya 1984 na 1991, akiwawekea historoa ya kutwaa mataji mawili ya Ligio Kuu msimu wa 1987 na 1990 na Kombe la Ulaya (UEFA Cup 1989).

Akifunga mabao 115 kwenye mechi 259, hata baada ya kuondoka mjini Naples 1991, alitengenezewa sanamu katika klabu hiyo akiwa kama Mungu wao, lakini kifo chake kimewachanganya mashabiki.

Kutokana na hilo, rais Aurelio de Laurentiis amethibitisha kwamba klabu yao itakaa kuangalia uwezekano wa kubadili jina la Uwanja wa San Paolo kwa ajili ya kumuenzi na kuuita jina lake.

“Tutaangalia uwezekano wa kuongeza jina lake katika uwanja, yaani tuuite San Paolo-Diego Armando Maradona,” De Laurentiis aliiambia chaneli ya michezo ya Ufaransa, RMC Sport.

Uamuzi huo umeungwa mkono na Meya wa Jiji la Naples, Luigi de Magistris, ambaye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter: “Tutabadili jina la Uwanja wa San Paolo kwa heshima ya Diego Armando Maradona!”

Kwa kutoa rambirambi zao kwa nguli huyo wa Argentina, meya aliongeza: “Diego Armando Maradona amefariki, mchezaji bora wa muda wote. Diego aliwafanya watu kuota ndoto ya kweli, aliiokoa Naples. 2017 alikuwa raia wa heshima. Diego, raua wa Naples na Argentina, ulitupa furaha. Naples inakupenda.”

Mamia ya mashabiki wa Napoli walikusanyika katika mitaa ya mji wao kuombeleza kifo cha nguli huyo atakayezikwa Alhamisi katika mji alikozaliwa, wakati rais wa Argentina akitangaza mapumziko ya siku tatu.