Nabi, Mayele wafichua siri

Tuesday September 28 2021
New Content Item (2)
By Thobias Sebastian
By Daudi Elibahati

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amefichua kuwa, alitenga muda wa kutosha kuwafutilia Simba ndio maana alieleza jambo la kuwa na uhakika kwa kiasi kikubwa kupata ushindi katika mechi yao, lakini pia akasema ujio wa Cedric Kaze nao umechangia kwa sehemu kubwa timu kuchangamka zaidi.

Nabi alisema awali alikuwa anasikia taarifa kutoka katika maeneo mbalimbali wamepanga kumfukuza katika nafasi hiyo ndani ya siku saba zijazo pamoja na kupewa michezo miwili.

Alisema taarifa ambazo hazikuwa nzuri kwake jambo lililomuongezea umakini mkubwa yeye na wenzake kufanya maandalizi sahihi na wachezaji wake ili kuona wanachukua taji la kwanza.

“Nadhani wakati huu kila mmoja atakuwa anasheherekea ushindi huu na kusahau mengine yote ya nyuma ila nikuambie tu ukweli kwa wachezaji ambao ninao ndani ya kikosi nikipata muda wa maandalizi ya kutosha timu hii ikawa na muunganiko tutakuwa hatari zaidi ya sasa katika mashindano ya ndani na nje ya nchi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Nilichofanya ili kufanikiwa kupata ushindi kwanza niliwaita wachezaji wangu wote na kuwambia umuhimu wa mechi hii na kila mmoja acheze kwa kujitolea na kuhakikisha tunashjinda kwani kulikuwa na mengi nyuma yetu,”

“Baada ya hapo niliwaangalia Simba ambavyo wanacheza msimu huu, kukosekana kwa wachezaji wake wawili tegemezi na mbinu za kocha wao ambaye namfahamu kwa muda mrefu. Baada ya kuyapata yote hayo nikayaamishia uwanjani katika uwanja wa mazoezi na siku ya mechi yenyewe jambo kubwa ambalo nimefurahishwa nalo wachezaji wangu si kushinda tu bali tulicheza vizuri katika kila ambalo nilihitaji.”

Advertisement

Pia alisema hatua kubwa ameipiga Yanga kwa kufanikiwa kuchukua taji lake la kwanza lakini akiwa na uhakika wa kupata muendelezo wa matokeo mazuri msimu huu.

“Najua wapinzani wetu Simba baada ya kushindwa kupata taji hilo watakwenda kuweka nguvu zaidi katika mas hindano ya ndani nasi kwa upande wetu tunaendelea kujipanga na kujiandaa ili kuwa bora zaidi yao,” alisema Nabi.

Naye nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto alisema katika msimu wake wa pili ndani ya kikosi hicho amefanikiwa kuchukua taji la pili si jambo dogo katika maisha yake ya soka.

Mwamnyeto alisema taji la kwanza ni ubingwa wa kombe la Mapinduzi ambalo hakuwepo lakini hilo la pili dhidi ya Simba alikuwa katika kikoso na kucheza dakika zote huku akiwa nahodha.

“Kama uliniona nilikuwa nacheza kwa kiwango cha juu zaidi ili kuwahamasisha wachezaji wenzangu na kuonyesha mfano wa nini cha kufanya nashukuru tumefanikiwa kupata kombe hili mbele ya Simba ambao inawachezaji wazuri,” alisema Mwamnyeto na kuongeza;

“Hatutaishia na furaha hii ya kuwafunga Simba pamoja na kuchukua hili taji la kwanza msimu huu kwani kulingana na kikosi kilivyo tunapambana zaidi ili kufikia malengo ya kuchukua ubingwa wa mashindano mengine ya ndani.”


MSIKIE MAYELE

Naye mfungaji wa bao la ushindi dhidi ya Simba, Fiston Mayele alisema kikosi chao kilistahili kupata ushindi katika mechi hiyo kubwa.

Mayele alisema Yanga walifanya maandalizi ya kutosha na kila mchezaji alikuwa na kiu ya kuanza vizuri kuchukua taji la kwanza ambalo litaongeza morali ya kushindana msimu huu.

Alisema mechi dhidi ya Simba haikuwa rahisi kwani walikutana na wachezaji ambao wanauwezo wa ushindani ulikuwa wa kutosha ndio maana kuna baadhi ya nafasi za kufunga mabao walishindwa kuzitumia.

“Kutokana na nafasi yangu ninayocheza jukumu la kwanza ni kufunga kwahiyo moyoni nilikuwa na malengo hayo ya kuhakikisha nafunga na kuisaidia timu yangu nashukuru hilo limetimia,” alisema Mayele na kuongeza;

“Unajua tulicheza mechi tatu mbili dhidi ya Rivers United na nyingine ile ya Zanacco zote tulishindwa kufanya vizuri kwahiyo tulikuwa na presha kubwa ya matokeo mazuri na mchezo huu wa Simba ulikuwa ndio mahala kwa kurudisha hali katika timu kwa kupata ushindi,”

“Tumefanikisha jambo kubwa la kupata ushindi ambalo kama timu tulikuwa tunahitaji lakini binafsi nimefikia malengo ya kufunga bao katika mchezo wangu wa kwanza wa kimashindano nikiwa na Yanga.”

Mayele alisema mara zote anapokuwa uwanjani hupenda kutimiza jukumu lake la kufunga na kama ikitokea ameshindwa kufanya hivyo basi awe msahada kwa mchezaji mwingine kufunga bao.

Alisema mpaka Yanga wameamua kumsajili pamoja na Heritier Makambo basi wanahitaji kuwa na safu kali ya ushambuliaji katika hawaendi tofauti na hilo kwa pamoja watambana na kulitimiza.

“Makambo ni mwenyeji hapa ndio maana napenda kumtolea mfano na kupitia kwake naimani atanisaidia katika mambo mengi ili kufanikisha kuwa na safu kali ya ushambuliaji Yanga msimu huu,” alisema Mayele na kuongeza;

“Kuhusu ushindani wa nafasi na Makambo hilo nadhani ni jukumu la kocha kuamua mchezaji atakayemtumia kati yetu au wote wawili.” alisema.

Advertisement