Nabi: Huyu Mayele mnamkosea hapa

FISTON Mayele yuko kwenye moto mkali akiendelea kutikisa nyavu za wapinzani lakini kama unafurahia mabao yake basi kocha wake Nasreddine Nabi ameshtua akisema bado kuna mabao zaidi anayaona na kwamba kuna kitu wenzake wanamkosea.

Akizungumza na Mwanaspoti Nabi alisema Mayele ameendelea kufunga kitu ambacho kwenye timu yao kila mmoja anafurahia lakini kuna namna wanamkosea kutokana na kuchelewa kumpa krosi anazozitaka.

Nabi alisema mbali na ubora wa Mayele katika kufunga lakini pia ana kasi kubwa akijua kukimbia sawa na mawinga wake wa pembeni lakini kuna krosi zinachelewa kumfikia.

“Ukimuona Mayele anavyokimbia utagundua anajitahidi kupunguza kasi ili aendane sawa na wenzake lakini unakuta kuna wakati amefika wao bado hawajapiga krosi, hii tutaendelea kuiimarisha zaidi,”alisema Nabi.

“Kama wakirekebisha hili tutaona mabao mengi zaidi kwa Mayele. Anaweza kufunga mabao mengi msimu huu kama akiendelea na kasi hii, jambo zuri ni kwamba hata wenzake na sisi tukiona anafunga kila mmoja anafurahia, alisema Nabi.

Aidha Nabi alimtaka Mayele pia kuongeza utulivu katika kufunga zaidi huku akidai mchezo wa juzi Jumamosi ilibaki kidogo apige tena mabao matatu ‘hat trik’.

“Nafikiri na pia anatakiwa kuongeza utulivu ili akimbie zaidi katika ufungaji, najua huwezi kufunga katika kila nafasi lakini zipo nafasi ambazo zinahitaji aongeze utulivu zaidi.”

Mayele mpaka sasa katika mechi 12 ameshafunga mabao 10 akiwa na hat trik moja na kuongoza msimamo wa wafungaji akifuatiwa na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao manane Sixtus Sabilo akiwa na mabao saba.


AMPA TANO KISINDA

Wakati mashabiki wakimuandama winga wao, Tuisila Kisinda, Nabi ameibuka na kumkingia kifua akisema wala hana tatizo na Mkongomani huyo akidai anazidi kuimarika tofauti na alivyofika.

Nabi alisema Kisinda amekuwa na maendeleo mazuri na bado eneo moja tu la maamuzi ambalo amekuwa akichelewa kufaya uamuzi wa mwisho kukamilisha kazi yake bora.

“Nimeona wanamlaumu sana (Kisinda) nafikiri wanatakiwa kumuacha, ukikumbuka ubora wake wakati anafika na sasa utagundua anazidi kuimarika, kuna makosa madogo ya maamuzi tu ambayo tutaendelea kuyafanyia kazi zaidi.

“Utaona mechi iliyopita alitengeneza bao lakini jana (juzi) akafunga ingawa waamuzi wamemkatilia, sikuona shida ya lile bao, akishaimarika katika kufanya maamuzi watu watanyamaza tena.”

Yanga imeondoka jana Jumapili usiku ikielekea jijini Mbeya ikiwafuata wenyeji wao Ihefu katika mchezo mwingine wa 13 wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Novemba 29,2022.