Nabi asaini mwaka na nusu Yanga

KOCHA mpya wa Yanga, Nasreddin Nabi amesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu wa kuitumikia klabu hiyo.

Mkataba huo amesaini leo baada tu ya kuwasili nchini na moja kwa moja alienda katika makao makuu ya klabu hiyo na kufanya tukio hilo.

Kaimu makamu mwenyekiti wa Yanga, Haji Mfikirwa amesema  wamempa mkataba huo Nabi na baada ya hapo wanaweza kumuongezea katika kuendelea na kazi.

“Tumempa mkataba wa mwaka mmoja na nusu baada ya hapo tutaendelea kuongezeana mkataba, ataanza kazi mara moja lakini kwa kushirikiana na Mwambusi (Juma).”

Mfikirwa alisema ujio wa kocha huyo utakuwa na benchi lake akiwa na Kocha Msaidizi Sghir Hammadi na wanafanya hivyo ili aweze kufanya vizuri.

“Safari hii kocha anakuja na benchi lake lote, baada ya hawa atakuja kocha wa viungo muda wowote kuanzia sasa ili kuja kufanya nae kazi.”

Mfikiliwa amesema makocha wote ambao wanakuja walishafanya nae kazi hapo awali katika klabu mbalimbali alizofundisha.

Nabi amesema amefurahia kujiunga na timu hiyo na kuwahakikishia mataji zaidi; "Nina furaha sana kuwa hapa, Yanga ni timu kubwa na nina matarajio makubwa ndani ya timu hii”