Nabi arudi Dar kumsoma Manula

YANGA ipo Zanzibar kwa kambi fupi kujiweka sawa na juzi usiku waliwachapa Mlandege bao 1-0.

Lakini jana kocha wao, Nasreddine Nabi alirejea Dar kushuhudia mechi ya leo baina ya Taifa Stars na DR Congo kuwania kufuzu Kombe la Dunia.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti linazo ni kwamba Nabi anakuja kusoma zaidi ubora wa wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho hususan wale wa Simba anayocheza nayo kwenye mechi ya watani mwezi ujao.

Lakini yeye amelizuga Mwanaspoti kwamba anakuja kuangalia wachezaji wake walioko kwenye timu hiyo.

Nabi alisema anaamini katika kikosi cha Stars mastaa wake viungo Feisal Salum, Zawadi Mauya; mabeki Dockson Job, Bakari Mwamnyeto, Kibwana Shomari na kipa Ramadhan Kabwili wapo ambao watapata nafasi ya kucheza akitaka kuangalia viwango vyao.

“Nataka kuangalia hiyo mechi. Nataka kuwafuatilia wachezaji wangu watakaopata nafasi ya kucheza katika timu ya Tanzania,” alisema Nabi ambaye hata kwenye mechi ya Simba na Namungo alikuwa kwenye Uwanja wa Mkapa akagundua baadhi ya mambo ambayo amekwenda Zanzibar kuyafanyia kazi.

Alisema katika kikosi cha DR Congo pia anataka kumfuatilia beki wake Djuma Shaban lakini pia mastaa wengine wanaocheza soka la Afrika.

“Kuna Djuma pia katika timu ya Congo ni vizuri kuwaangalia wote kama atapata nafasi. Kuna wachezaji wengine wanaocheza Afrika nitawaangalia katika timu ya Congo unajua nafasi kama hii ndio tulimuona Fiston Mayele,” alisema.