Nabi apiga mkwara Yanga

YANGA wanashuka Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza leo wakiwa wageni wa Biashara United, lakini vinara hao wa Ligi Kuu Bara waliobakiza pointi nne tu kuwa mabingwa wameonyesha hawana huruma wakishusha mkwara mzito.

Yanga itashuka kwenye dakika 90 hizo ikiwa na hesabu mbili kubwa, kwanza wakitaka kushinda ili kubakisha pointi moja tu kutwaa taji lao la 28 la Ligi Kuu, pia watahitaji ushindi mzuri utakaoongeza morali yao kabla ya kukutana na watani wao Simba.

Klabu hizo kongwe mbili zitakutana kwenye uwanja huo Jumamosi Mei 28, katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambao hautakuwa na sare kwa namna yoyote lazima mmoja ang’oke.

Jumamosi Mei 21, usiku tayari Yanga ilishatua Jiji la Mwanza ikitokea Dar es Salaam ambako siku moja kabla ya safari iliiangamiza timu nyingine iliyepo mkiani mwa msimamo Mbeya Kwanza kwa mabao 4-0 na kuzidi kubariki presha yao ya kushuka daraja.

Biashara United pia hali yake sio nzuri na kitu kibaya zaidi kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameshatamka kwamba hatakuwa na huruma ya kupanga kikosi dhaifu kwa kuwa anaelekea kukutana na Simba.

Nabi amesafiri na jeshi lake lote hadi wachezaji wagonjwa akiwemo Yacouba Sogne ambaye hajacheza msimu huu, huku kile kikosi chake cha kwanza kikiwa salama tayari kwa mchezo huo.

Mbali na Yacouba, Nabi katika mchezo uliopita aliwapumzisha baadhi ya nyota wake ambao ni Djuma Shaban, Feisal Salum na Bakari Mwamnyeto wote wa kikosi cha kwanza aliosema watatumika mechi zijazo ikiwemo hii ya leo.

“Hata Sure Boy (Salum Abubakari) na yeye niliamua kumtoa kwa sababu alicheza chini sana kutokana na kutumia nguvu nyingi mchezo uliopita, namuhitaji kwenye mechi zijazo na yeye ndio maana nilimpumzisha,” alisema Nabi.

Alisema lengo lao kubwa msimu huu ni kuwa mabingwa na hata kama wako mbali lakini wana kila sababu ya kushinda ili wazidi kulisogelea taji hilo ambalo walilikosa kwa miaka nne mfululizo.

“Ndio, tumekuja kamili kwa malengo ya ushindi wa mchezo huu, tumefanya mazoezi ya kwanza vizuri leo (jana) hapa Mwanza na sasa tunausubiri mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Biashara United,” alisema Nabi na kuongeza:

“Hatutakiwi kudharau timu yoyote bado hatujawa mabingwa ingawa hesabu zinatubeba, akili ya kusema tutapanga timu dhaifu kwa kuwa tunakwenda kukutana na Simba, hapana hilo halipo katika akili yetu, nimewaambia wachezaji mchezo wetu muhimu na mkubwa sasa ni huu wa Biashara tunatakiwa kuwaheshimu bila kuangalia wako wapi kwenye ligi.”

Wakati Nabi akiyasema hayo Biashara wao hali yao haiko sawa baada ya kutoshinda mechi tano mfululizo wakipoteza zote sasa wanatakiwa kuwa makini wakikutana na anayeongoza ligi.

Kocha wa Biashara, Vivien Bahati alisema anafahamu hawako katika nafasi nzuri pia wakikutana na timu inayocheza sana soka la kushambulia lakini wamejipanga kuhakikisha wanarudi kwenye ramani ya ushindi kaunzia mechi hii ya leo.

“Tunakutana na Yanga ni kubwa na ngumu lakini Biashara tuna hesabu zetu katika kujiondoa kule tulipo, tumekuwa katika maandalizi makubwa tukitambua tunakwenda kukutana na timu inayocheza soka la kushambulia zaidi,” alisema Bahati ambaye ni kocha wa zamani wa Azam FC.