Mzambia anatua Simba, Luis anasepa

Tuesday June 22 2021
luis pic
By Thobias Sebastian

WAKATI wakiendelea kukuna vichwa kuhusu ofa nzito zilizopo mezani mwao juu ya dili la winga wao nyota, Luis Miquissone ili apishane na Mzambia Moses Phiri, mabosi wa Simba wametua kwa kiungo fundi kutoka Guinea kwa lengo la kuboresha kikosi chao kwa msimu ujao.

Jumatano iliyopita Bodi ya Wakurugenzi Simba ilikutana jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali ikiwamo usajili wa msimu ujao pamoja na mikakati ya kumaliza msimu huu kwa kishindo, kisha kupeana majina ya nyota wanaowahitajika kikosini.

Wajumbe wa Bodi hiyo ya Simba, pia walikuwa wakijadili ofa zilizopo mezani mwao kutoka timu za Ulaya na Afrika Kaskazini, ikiwamo Al Ahly ya Misri na CR Belouzidad ya Algeria juu ya kumtaka winga wao, Luis ili kuona dili lipo walikubali ili winga huyo kutoka Msumbiji auzwe.

Awali mabosi hao wa Simba walikuwa wakikazia, kutaka kumzuia Luis asiondoke Msimbazi, lakini baada ya kuona misuli wa fedha walizonazo timu zinazomhitaji wameamua kulegeza masharti yao na kuziambia klabu hizo kama kweli wanamtaka basi wajiandae kutoa mkwanja mrefu.

Simba imeweka dau lisilopungua Dola 600,000 na wakati wakisikilizia klabu hizo, pia wameanza harakati za kutafuta mbadala wake, ambaye jina walilonalo ni la Moses Phiri ambayeWekundu wamekubali kuipa klabu yake ya Zanaco fedha pamoja na mchezaji mmoja kwa mkopo.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, viongozi hao wamekubaliana mbadala wa Luis lazima awe Phiri, aliyeingia kwenye rada za Simba, huku timu yake ikielezwa ipo tayari kumtoa kama italipwa fedha na kuongezewa Perfect Chikwende ili akaichezee kwa mkopo.

Advertisement

“Biashara ya kumpata Phiri tunataka kuifanya kwa kuwapa Zanaco, fedha pamoja Chikwende kwa mkopo lakini hii endapo Luis ataondoka, kwani tayari tutakuwa na fedha tuliokubaliana nao,” kilisema chanzo makini kutoka Simba kilichoomba kuhifadhiwa jina na kuongeza;

“Mbali na dili hilo la Luis kupishana na Phiri, pia tumeanza msako wa kiungo mkabaji anayetokea Guinea. Jamaa ametuvutia ila tunashindwa kutaja jina kwa saa kwa vile hatujaanza naye lolote ila tumemuona na tunataka kumsikia kocha Didier Gomes naye atoe msimamo wake kwake.”

“Kama unakumbuka awali kulikuwa na kiungo kutoka Mali, aliyependekezwa na Gomes, ila nasi tukasema kuna wawili tutawaleta ili kuona yupi ni bora kati ya hao ili tumchukue sasa mmoja kati ya hao ndio huyo Mguinea,” chanzo hicho kiliongeza.

Mapema uongozi wa Simba kupitia kwa Makamu wa Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema wapo tayari kumuachia Luis kama klabu zinazomtaka zitafikia dau waliloliweka na kubwa ni kutaka kuona wanaijenga Simba kali zaidi ili kupata mafanikio zaidi ya msimu huu.

“Huo ndio msimamo wetu kama kuna timu yoyote kati ya hiyo ambazo zinamhitaji Luis Miquissone itakubali kutupatia kiasi hicho cha pesa tutawachia,” alikaririwa.

Advertisement