Mwamuzi Simba, Al Ahly huyu hapa

REFA wa kimataifa wa Cameroon, Sidi Alioum, ndiye atakayechezesha mchezo wa raundi ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kesho baina ya wenyeji Simba na Al Ahly ya Misri utakaochezeshwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini kuanzia saa 10.00 jioni.

Alioum aliyechezesha mchezo wa fainali ya mashindano ya mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019 nchini Misri baina ya Algeria na Senegal, atasaidiwa na refa msaidizi namba moja, Elvis Guy Nguegoue, refa msaidizi namba mbili, Carine Atezambong Fomo na refa wa nne wa akiba,  Jeannot Franck Bito ambao wote wanatoka Cameroon.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni David Gikonyo Mwangi kutoka Kenya wakati msimamizi mkuu atakuwa ni Victor Lawrence Lual Lual wa Sudan.

Mchezo huo utakuwa na mtathmini wa kiufundi wa masuala ya luninga ambaye amepangwa kuwa Bechir Hassan kutoka Tunisia wakati huohuo Limbanga Manfred Kinyero kutoka Tanzania akiteuliwa kuwa Ofisa wa masuala ya vipimo vya ugonjwa wa Covid-19

Refa Sidi Alioum mbali ya kuchezesha mechi ya fainali ya Afcon mwaka 2019, pia kwa nyakati tofauti amekuwa akipata fursa ya kuteulizwa kuchezesha michezo ya mashindano mbalimbali makubwa nje na ndani ya bara la Afrika.

Mwaka 2014, alichezesha Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Brazil na kuweka rekodi ya kuwa refa mdogo zaidi katika mashindano ya mwaka huo lakini pia amewahi kuchezesha Kombe la Dunia la Klabu, Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya umri wa miaka 20 na pia Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17.

Mwaka 2018, refa huyo aliibuka mshindi wa tuzo ya mwamuzi bora nchini Cameroon na anatajwa kuwa miongoni mwa marefa bora kuwahi kutokea nchini humo.