Mwakinyo apanda viwango vya ngumi duniani, afikisha nyota tatu

Mwakinyo awa wa 43 duniani, afikisha nyota tatu

Muktasari:

  • Mwakinyo aliyewahi kuwa bondia namba 14 wa dunia baada ya kumchapa Sam Eggington nchini Uingereza mwaka 2018 aliporomoka mwaka jana hadi nafasi ya 86.

BONDIA Hassan Mwakinyo amepanda hadi nafasi ya 43 kwenye viwango vya ngumi vya dunia.

Bondia huyo namba moja nchini ametajwa kuwa bondia wa nyota tatu duniani, akihitaji kutafuta nyota nyingine mbili ili kuingia anga za mabondia wanaotamba duniani akiwamo Manny Pacquiao mwenye nyota tano.

Kwa mujibu wa viwango vilivyotolewa na mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia saa chache zilizopita leo Jumatano Novemba 25,2020, Mwakinyo amepanda kutoka nafasi ya 78 hadi ya 43 duniani kati ya mabondia  2,050 wa uzani wa super welter.

Mwakinyo aliyewahi kuwa bondia namba 14 wa dunia baada ya kumchapa Sam Eggington nchini Uingereza mwaka 2018 aliporomoka mwaka jana hadi nafasi ya 86.

Bondia huyo licha ya kushinda mapambano kadhaa mwaka huu likiwamo la Tshibangu Kayembe, alibaki nafasi ya 78 mpaka leo vilipotajwa viwango vipya na kupanda hadi nafasi ya 43.

Summary.
Mwakinyo amecheza mapambano 20 na kushinda 18 huku akichapwa mara mbili tangu alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.

________________________________________________________________

Na Imani Makongoro