Prime
MVP aziingiza vitani Simba, Yanga
MCHEZAJI Bora wa Ligi ya Kenya (MVP), msimu wa huu, Mghana Enock Morrison anayecheza Gor Mahia FC ya Kenya, amekuwa lulu sokoni, baada ya vigogo wa soka hapa nchini wa Yanga, Simba, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United kumuhitaji.
Awali Singida ili kuwa timu pekee iliyohitaji saini ya nyota huyo tangu dirisha dogo la Januari 2026, ingawa baada ya kiwango bora alichokionyesha akiwa na Gor Mahia, kimeanza kuzivutia klabu tano za Tanzania kwa ajili ya msimu ujao.
Chanzo kutoka ndani ya Singida, kimeliambia Mwanaspoti, Enock ni miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa ukaribu na Singida, ambapo tayari mazungumzo ya awali yalianza kufanyika tangu kwenye dirisha dogo la Januari 2026.
“Dirisha dogo la Januari 2026, tulifikia makubaliano na mchezaji mwenyewe, ila tulipokwenda kwenye klabu yake kwa ajili ya kufikia muafaka tukashindwana kutokana na baadhi ya vipengele, japo kwa sasa tunarudi tena upya,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa taarifa huyo amesema licha ya kukabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa timu nyingine, ila wataendelea kupambana kwa ajili ya kuipata saini yake, baada ya mchezaji mwenyewe pia kuonyesha nia ya kujiunga na kikosi hicho cha Singida.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TRA United, Charles Obiny aliliambia Mwanaspoti kwa sasa hawajapokea taarifa yoyote ya usajili kutoka kwa benchi la ufundi chini ya Kocha, Mrundi Etienne Ndayiragije kwa sababu bado msimu huu haujaisha.
Licha ya kushinda mchezaji bora wa msimu yaani (MVP), ila Enock alishinda pia tuzo ya kiungo bora wa msimu wa Ligi Kuu ya Kenya, huku akiisaidia Gor Mahia kutwaa ubingwa, baada ya kufikisha pointi 69, wakifuatiwa na AFC Leopards (pointi 64).
Katika Ligi Kuu ya Kenya msimu huu, nyota huyo alichangia mabao saba ya Gor Mahia FC baada ya kufunga matatu na kuasisti manne, huku akiibuka pia kidedea kwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi, baada ya kufanya hivyo mara 15.