Mtibwa yaichapa Transit, Hilika atupia hat-trick

MTIBWA Sugar wamepata ushindi wa 4-1 dhidi ya Transit Camp katika mchezo wa kwanza mtoano kwa ajili ya Ligi Kuu msimu ujao uliochezwa leo uwanja wa Uhuru.

Wakati Mtibwa wakipata ushindi huo mshambuliaji wake, Ahmada Hilika alifunga mabao matatu (Hat-trick).

Trans walianza mpira kwa spidi kwenye kipindi cha kwanza lakini changamoto kubwa ilikuwa kwenye upande wa kushambulia.

Upande wa Mtibwa walikuwa watulivu hasa kwenye eneo la ushambuliaji alilokuwa anacheza Kelvin Sabato na Ahmada Hilika.

Washambuliaji hao walikuwa wanacheza sambamba na presha kubwa ya mabeki wa Transit ambao walikuwa wanatumia zaidi mabavu.

Dakika ya nane Mtibwa Sugar walipata bao la kwanza kupitia kwa Ahmada Hilika baada ya Salum Kanoni kupiga krosi iliyounganishwa kwa kichwa na Kelvin Sabato na Hilika alipiga shuti na mpira kwena wavuni.

Bao hilo lilionekana kuwapa nguvu Mtibwa huku Trans wakiwa wanajipanga upya kupanga mashambulizi lakini hawakupata bao.

Dakika 12 Sabato aliifungia bao la pili Mtibwa baada ya George Makang’a kuingia na mpira ndani ya boksi na kufyatua shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Transit Camp, uharaka wa Sabato alionganisha mpura huo kwa kichwa na kwenda wavuni.

Dakika 15 Trans Camp walisawazisha bao ambalo mshambuliaji wake Karegea Hazanga, aliutuliza mpira na kuupiga wavuni huku kipa Abdultwalib Msheri akibaki mdomo wazi.

Baada ya bao hilo mchezo ulitulia na timu zote zilikuwa zikicheza kwa utulivu wakitafuta mbinu ya kupenya kwenye safu ya ulinzi kwa mpinzani wake.

Katika kipidi cha pili Trans walianza kwa presha na kuonyesha kutaka kupata bao la kusawazisha lakini hawakufanikiwa.

Dakika 50 Transit walifanya mabadiliko ya kutoka Hassan Gumbo na kuingia Shafih Moshi kwenda kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji akitokea pembeni.

Trans walionekana kubadilika na kupeleka mashambulizi mara kwa mara langoni kwa Mtibwa ila kupenya safu ya ulinzi ilikuwa tabu.

Dakika 55 winga wa Trans, Karegea Wazanga alifanyiwa madhambi pembeni kidogo ya boksi, mashabiki walipiga shangwe iwe penalti lakini haikuwa hivo.

Dakika 57 Prosper Pius alitolewa na kuingia  Samwel Kamuntu kwenda kukngeza nguvu eneo la ushambuliaji ambalo lilionekana kusua sua, wakati huo huo Mtibwa alitoka Kelvin Sabato na kuingia Salum Kihimbwa.

Wachezaji wa Mtibwa spidi yao ilikuwa inapungua kadri mpira ulivyokuwa unachezwa, wachezaji wa Trans walikuwa wanatumia faida hiyo lakini hawakupata bao.

Dakika 68 Trans walifanya mabadiliko mengine ya kumtoa Athuman Kisatu na kuingia Masume Mashauri.

Mtibwa ilipata bao la tatu dakika 70 kupitia kwa Ahmada Hilika aliyeunganisha vizuri kwa kichbwa krosi ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’.

Mtibwa waliongeza mashambulizi na dakika 85 Ahmada Hilika alifunga bao la nne baada ya kupiga shuti kali nje ya boksina mpira kwenda wavuni.