Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtibwa ilivyojenga mashine za maana

Shaaban Kado

Muktasari:

Timu hii iliyoanzishwa mwaka 1988 na baadhi ya wafanyakazi wachache wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa Sugar Estates Ltd, uanzishwaji huu wa timu ulikuwa kama utani lakini baadaye mwaka 1989 ikaanza kushiriki Ligi Daraja la Nne.

MTIBWA Sugar ndiyo klabu inayoongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 15 na kuzipiku timu nyingine 13 zinazoshiriki msimu huu wa ligi hiyo. Timu hii inatokea katika mashamba ya miwa huko Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Timu hii iliyoanzishwa mwaka 1988 na baadhi ya wafanyakazi wachache wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa Sugar Estates Ltd, uanzishwaji huu wa timu ulikuwa kama utani lakini baadaye mwaka 1989 ikaanza kushiriki Ligi Daraja la Nne.

Baada ya kupambana kwa muda mrefu Mtibwa ikapanda Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1996 na miaka miwili baadaye mfumo wa ligi ukabadilika kuwa Ligi Kuu. Kutokana na kujituma kwa wachezaji wake, Mtibwa ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu mwaka 1999 lakini kwa pointi za mezani baada ya kuipiku Yanga katika baadhi ya rufaa zake.

Mwaka 2000 tena ulikuwa wa Mtibwa kwani ilifanikiwa kutwaa ubingwa kwa mara nyingine, timu hii ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la CAF (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) katika miaka ya 2000, 2001 na 2002. Pia ilishiriki Kombe la Shirikisho mwaka 2004, kote huko iliishia raundi ya kwanza isipokuwa mwaka 2000 na 2002 ilipofanikiwa kuvuka raundi ya pili.

Mtibwa ni miongoni mwa klabu zilizotoa wachezaji wengi katika Ligi Kuu, ambao sasa wametapakaa katika klabu nyingine ndani na nje ya nchi wakicheza soka. Kama timu hiyo ingekuwa imara kiuchumi na kudhibiti kikosi chake kisisambaratike au wachezaji wake kununuliwa na timu pinzani ingetisha zaidi na pengine kutwaa ubingwa.

Wachezaji wengi waliopitia Mtibwa wanafanya vizuri kwa sasa kwenye timu zao na kama haitoshi Simba na Yanga zimerudi tena Manungu kusaka wachezaji wengine kwenye dirisha dogo. Angalia orodha ya wachezaji wafuatao;

Shaaban Kado

Kipa Shaaban Kado bado yupo katika kiwango chake naye ni mmoja wa wachezaji waliopitia Mtibwa na kuitangaza vizuri klabu hiyo ndani na nje ya nchi. Kado baada ya kufanya vizuri akiwa na Mtibwa alisajiliwa Yanga ambako hakudumu sana na sasa yupo Coastal Union ya Tanga. Kutokana na uwezo wake, Kado aliichezea Taifa Stars na Kilimanjaro Stars lakini hayupo kwenye timu ya Taifa kwa sasa kutokana na kuyumba kwa timu yake kwenye ligi katika siku za karibuni.

Hussein Sharrif ‘Casillas’

Huyu ni kipa namba mbili katika klabu ya Simba ambaye msimu uliopita alikuwa kipa bora akiwa na Mtibwa, lakini msimu huu amesajiliwa na Wekundu wa Msimbazi japokuwa hana uhakika wa nafasi kikosi cha kwanza. Amewahi kuitwa Taifa Stars mara kadhaa lakini hakuwa na nafasi kikosi cha kwanza. Bado ana nafasi ya kufanya vizuri katika soka ndani na nje ya nchi.

Juma Abdul

Beki wa kulia Juma Abdul amejihakikishia namba katika kikosi cha Yanga akiwa anacheza kwa bidii na kujituma kwa muda wote kiasi cha kumvutia Kocha Marcio Maximo kwani aliyekuwa anaishikilia nafasi hiyo Mbuyu Twite sasa anachezeshwa kama kiungo mkabaji. Twite alianza kucheza nafasi hiyo baada ya Frank Domayo kuondoka na kujiunga na Azam FC.

Issa Rashid ‘Baba Ubaya’

Beki wa kulia Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ wa Simba naye ametokea Mtibwa akajiunga na klabu hiyo. Akiwa Mtibwa, Baba Ubaya alipata nafasi ya kuitwa katika timu za taifa za vijana na ndipo nyota yake ilipong’aa na kufuatiliwa na klabu kubwa lakini Simba ndiyo iliyofanikiwa kumsajili. Hata hivyo kwa sasa nafasi yake ni finyu katika kikosi cha Simba na kutoa nafasi kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Salvatory Ntebe

Wakati fulani wakati Marcio Maximo bado anaifundisha Taifa Stars na Kilimanjaro Stars alikuwa akimuita beki Salvatory Ntebe wakati akichezea Mtibwa kutokana na ubora wake, sasa beki huyu yupo Ruvu Shooting anakocheza kama beki wa kati lakini ni zao la Mtibwa.

Abdulhalim Humoud

Alianza kung’ara akiwa na Ashanti United akaitwa hadi Taifa Stars wakati wa Marcio Maximo lakini baadaye akatua Mtibwa ambako hakucheza sana kabla ya kusajiliwa na Simba ambako alicheza kwa vipindi viwili tofauti na sasa anacheza soka kwenye klabu ya Sofapaka ya Kenya.

Kiggi Makassy

Kiungo Kiggy Makassy ameibuliwa na Kocha Marcio Maximo ambaye alikuwa na mpango wake kabambe wa kukuza vijana ndipo Mtibwa walipomuona na kumsajili katika kikosi chao ambako alicheza kwa muda kisha akajiunga na Yanga.

 Baadaye akajiunga na Simba hadi alipoumia mwanzoni mwa msimu uliopita, sasa amepona na anafanya mazoezi na Azam akitarajia kujiunga na timu mojawapo ya Ligi Kuu mwakani.

Said Bahanuzi

Straika Said Bahanuzi ambaye wengi hupenda kumuita jina la utani la straika wa Kombe la Kagame baada ya kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo mwaka 2012 hapa nchini, naye ni zao la Mtibwa ambalo sasa lipo Yanga.

Alitamba na Mtibwa na kuwa mwiba mkali kwa Simba na Yanga kila alipokutana nazo lakini tangu alipotua Yanga ameshindwa kuendeleza cheche zake na sasa anaweza kujiunga na Stand United ya Shinyanga inayoshiriki Ligi Kuu.

Abdallah Juma

Abdallah Juma ni straika aliyeichezea Mtibwa kwa muda kisha akasajiliwa Simba lakini mambo hayakumwendea vizuri akaona isiwe shida akarejea tena katika klabu yake na yupo hadi sasa akiichezea timu hiyo japokuwa hana nafasi ya maana kikosi cha kwanza.

Monja Liseki

Hakuna anayekosea, lakini ukitaja jina Monja Liseki kila mtu anashtuka kuanzia shabiki wa soka la uswahilini hadi yule wa Ligi Kuu kwani ameifanyia mengi Mtibwa na hata alipokuwa anaichezea Sigara wakati huo.

Huyu amewahi kuichezea Simba lakini akaenda Mtibwa ambako amecheza kwa muda mrefu hadi alipoondoka miaka mitatu iliyopita na sasa amejisajili Mwadui FC ya Shinyanga inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Hussein Javu

Hiki ni kifaa kingine cha Mtibwa ambacho kimepitia klabu za Simba na Yanga na akasajiliwa na Yanga lakini sasa mambo ni magumu kwake kwani hana nafasi kikosi cha kwanza. Javu akiwa Mtibwa alikuwa anazitesa Simba na Yanga na kuonekana bonge la straika lakini kama ilivyo kwa wenzake, sasa hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga lakini bado anapendwa na kocha Maximo.

Shaaban Kisiga

Muite Shaaban Kisiga lakini wengi humuita Marlone kama jina lake la utani, huyu ni kiungo mwenye mambo mengi uwanjani na aliyecheza soka kwa muda mrefu katika klabu kubwa nchini isipokuwa Yanga tu.

Amewahi kucheza SC Villa ya Uganda, Simba halafu akaenda Azam FC kisha Oman na baadaye akajiunga na Mtibwa kabla ya kurejea Simba msimu huu. Huyu ana bahati mbaya kwani sasa amesimamishwa kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu.