Mtanzania ashinda ubingwa wa IBF, IBO Australia

Bondia Mtanzania, Bruno Tarimo 'Vifua Viwili' ametawazwa kuwa bingwa wa mataji wa mikanda ya kimataifa ya IBF na IBO nchini Australia leo Jumatano.

Saa chache zilizopita majaji wote walimpa ushindi bondia huyo mzaliwa wa Kilimanjaro dhidi ya mwenyeji, Kye MacKenzie.

Majaji wawili walitoa pointi 97-93 kila mmoja na jaji namba tatu alitoa pointi 96-94 kwa Bruno kwenye pambano hilo la raundi 10 la uzani wa super feather lililopigwa kwenye ukumbi wa WIN Entertainment Centre, Wollongong, New South Wales, Australia.


Kwa ushindi huo sasa Bruno ametetea ubingwa wake wa kimataifa wa IBF na kutwaa ubingwa wa mabara wa IBO.

Ushindi huo utampandisha zaidi Bruno kutokana na ubora wa mpinzani wake ambaye kabla ya kipigo cha leo alikuwa wa 47 duniani akimuacha kwa nafasi 17 Bruno kwenye uzani wa super feather.

"Hii ni habari njema kwa Tanzania, Bruno amekuwa na rekodi nzuri tangu alipoanza kuishi Australia mwaka 2018," alisema Anthony Rutha miongoni mwa wakuzaji wa ngumi za kulipwa nchini.