Msimu wa tatu mbio za Lake Viktoria wazinduliwa, wakimbiaji 1,400 kuchuana

Muktasari:
- Mbio zilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2021 zikianza na wakimbiaji 300, msimu wa pili zikafikisha wakimbiaji 1,000 na msimu zinatarajia washiriki 1,400 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa
Mwanza. Msimu wa tatu wa mbio za Lake Viktoria maarufu kama 'Transec Lake Victoria Marathon' umezinduliwa rasmi leo jijini Mwanza ambapo wakimbiaji 1,400 watashiriki huku faida za mbio hizi zikitarajiwa kuwanufaisha watoto wenye mahitaji maalum.
Uzinduzi huo umefanyika leo Mei 26, 2023 Mwanza na zitafanyika Julai 2, mwaka huu jijini hapa zikishirikisha wakimbiaji kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo fedha zitakazochangwa na washiriki zitasaidia kuwatibu watoto wenye saratani katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, Bugando.
Mratibu wa mbio hizo, Halima Chake, amesema msimu uliopita ulioshirikisha wakimbiaji 1,000 ulifanikisha kuwakatia bima za afya watoto 85 wenye mahitaji maalum wanaolelewa katika kituo cha Watoto Afrika cha Buswelu, Mwanza.
Amesema mbio zitakazoshindaniwa ni Kilometa 2.5 kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10, Kilometa 5, Kilometa 10 kwa makampuni mbalimbali na kilometa 21.1, ambapo usajili umefunguliwa rasmi huku akitoa wito kwa wakimbiaji wote kujisajili kwa wingi ili kufanikisha lengo lililokusudiwa.
"Kwa kilometa 2.5 kiingilio ni Sh 20,000, km 5 ni Sh 30,000, km 10 ni Sh 35,000 sawa na km 21.1, mazoezi ni muhimu sana katika maisha yetu siyo tu kwa ajili ya muonekano bali kuimarisha afya," amesema.
Akizindua mbio hizo, Katibu Tawala Msaidizi Uwekezaji na Biashara mkoa wa Mwanza, Patrick Karangwa amesema marathoni hiyo inautangaza mkoa huo, kuhifadhi Ziwa Viktoria na kuchochea biashara na kukuza utalii.
"Mkoa tutatoa ushirikiano kuzikuza mbio hizi ziwe kama zile za Kilimanjaro na tunaziomba kampuni za kizawa kuunga mkono kwani zina manufaa kiafya na mchango mkubwa kwenye jamii," amesema Karangwa
Mmoja wadhamini wa mbio hizo, Victor Okeyo amesema wameunga mkoni ili kuimarisha afya na kurudisha faida kwa jamii ya Kanda ya Ziwa ambayo imekuwa sehemu kubwa ya mafanikio ya shughuli zao za migodini na viwandani.
Mwakilishi chama cha Riadha Mwanza, Kulwijira Malima amesema "mbio hizi ni za wazawa ni jukumu letu kuwaunga mkono kufanikisha jambo hili, chama chetu kitasaidia kuratibu mbio na kushiriki vyema,"