Mshery wala habahatishi

YANGA msimu huu imefanya usajili wa maana kila idara yenye uhitaji na wachezaji wapya wamezidi kuonyesha uwezo huku kipa Aboutwalib Mshery akifunguka habahatishi.

Kipa huyo alisajiliwa na Yanga dirisha dogo la usajili linaloendelea akitokea Mtibwa Sugar na hadi sasa ameidakia timu yake mpya kwenye michezo mitatu akionyesha uwezo mkubwa.

Mechi hizo ni ile ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, Desemba 31 mwaka jana ambayo Yanga ilishinda kwa bao 4-0 na nyingine ni mechi ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Taifa Jang’ombe na kushinda 2-0 na ile ya juzi dhidi ya KMKM uliomalizika kwa sare ya bao 2-2 na wakitinga nusu fainali.

Katika mechi hizo Mshery alionesha kiwango cha hali ya juu na kufanya mashabiki na wadau wa soka kumtabiria makubwa kwa siku za usoni.

Miongoni mwa mambo ambayo msheri alionesha kuyamudu zaidi ni kuweza kucheza mpira kwa miguu sambamba na mabeki wake huku akianzisha mashambulizi na kuifanya timu icheze kwa utulivu.

Awali katika moja ya mahojiano na Mwanaspoti, Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alieleza kuwa Yanga ya msimu huu inahitaji kipa mwenye uwezo mkubwa wa kutumia miguu kucheza na kuanzisha mashambulizi kama ilivyo kwa kipa namba moja wa timu hiyo, Djigui Diarra aliyeko Cameroon na timu yake ya taifa (Mali) kwenye michuano ya Afcon.

“Tunacheza kuanzia nyuma hivyo tunahitaji kipa awe na uwezo mzuri wa kucheza mpira kwa mguu na kontroo za kutosha ili aweze kurahisisha kazi kwa mabeki wake kama anavyofanya Diarra,” alisema Kaze.

Alipoulizwa kuhusu hilo, Msheri alifunguka habahatishi kwani alikuwa akifanya hivyo tangu yupo Mtibwa na kwenda kwake Yanga ni kuendeleza alipoishia tu.

“Huwa napenda kucheza hivyo, nimebahatika kuwa na matumizi mazuri ya miguu yote na kama uliangalia mechi zangu nyingi kipindi nipo Mtibwa nilikuwa nacheza sana hivyo,” alisema Mshery na kuongeza anashukuru kuja Yanga na atahakikisha anakuwa bora zaidi na kuisaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea.