Mpole: Simba imetuheshimisha


Muktasari:

  • Simba ilipata ushindi wa mabao 7-0 juzi dhidi ya Horoya ya Guinea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na kujihakikishia kwenda robo fainali ikiwa na mechi moja mkononi nyuma ya Raja Casablanca iliyokusanya pointi 13 na zitakutana Aprili Mosi.

KINARA wa mabao wa Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita, George Mpole anayekipiga FC Lupopo ya DR Congo kwa sasa amesema kutinga kwa Simba katioka hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika imeiheshimisha Tanzania na kutoa fursa kwa vijana kupata nafasi zaidi za kutoka nje ya nchi.

Simba ilipata ushindi wa mabao 7-0 juzi dhidi ya Horoya ya Guinea kwenye mechi ya Kundi C ya Ligi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na kujihakikishia kwenda robo fainali ikiwa na mechi moja mkononi nyuma ya Raja Casablanca iliyokusanya pointi 13 na zitakutana Aprili Mosi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mpole alisema mafanikio ya Simba yameifanya Tanzania iendelee kutoa timu nne kwenye mashindano ya kimataifa kutokana na pointi walizozikusanya zisizoweza kufikiwa na nchi nyingine yeyote na hiyo ni heshima kubwa kwa taifa.

"Simba inahitajika kutazamwa kwa jicho la pili imekuwa timu bora inayolifanya soka la Tanzania kuwa bora na kuwavutia mastaa mbalimbali kutoka nje kutamani kuja kucheza ligi yetu.

Pia imekuwa ikitazamwa sana hii ni fursa kwa wachezaji wa ndani pia kupata nafasi ya kuonekana na wao kutoka kwenda kujaribu maisha mengine nje ya ligi yetu amb ayo imekuwa bora na kuimarika zaidi," alisema Mpole aliefunga mabao 17 na kubeba kiatu msimu uliopita akiwa na Geita Gold.

Mpole alisema ni wakati wa serikali kuiangalia kwa jicho la karibu timu hiyo katika hatua hiyo ili kuipa motisha zaidi na wao kuendeleza ubora kwenye mashindano hayo. Yanga jana ilikuwa uwanjani kuivaa US Monastir ya Tunisia na kama ingepata ushindi nayo ingetinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Walichokifanya kwenye hatua ya makundi ni kitu sahihi kiliongeza ushindani kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe na timu kuweza kufikia lengo hilo linatakiwa kuendelezwa hatua inayofuata ikiwezekana kwa kuongeza dau ambalo litatoa chachu;

"Ubora wa Simba kwenye mashindano ya kimataifa umeifanya Yanga pia kujitafakari na wao kujipanga na kufanya vyema tofauti na misimu ya nyuma pia wakitinga hatua hiyo wanahitaji motisha zaidi ili kuendelea kukuza soka la Afrika." alisema Mpole.