Moloko, Saido wote mtegoni

KIWANGO bora kilichoonyeshwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na winga Denis Nkane katika Kombe la Mapinduzi kinawalazimisha Jesus Moloko na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kufanya kazi ya ziada ili waendelee kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga.

Uwezo wa nyota hao wawili waliosajiliwa na Yanga kucheza katika nafasi ambazo Ntibazonkiza na Moloko wanacheza hivi sasa na namna walivyoanza vyema katika Kombe la Mapinduzi ni mambo mawili ambayo yanawaweka katika nafasi kubwa ya kushindania nafasi katika kikosi cha kwanza tofauti na nyota wengine wawili kati ya wanne waliosajiliwa ambao hawaonekani kama wanaweza kuchukua nafasi ya nyota wanaoanza kikosini pindi ligi itakaporejea.

Winga Denis Nkane aliyenaswa kutokea Biashara United ameonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia kutokea pembeni, kupiga krosi na pasi za hatari pamoja na kufunga jambo linalomuweka katika nafasi nzuri ya kumtibulia Ducapel Moloko.

Nkane pia ameonyesha kuwa na kasi kubwa na uwezo wa kumiliki mpira na licha ya ugeni wake, ameonekana kucheza kwa kujiamini jambo lililomfanya awe kivutio kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

Kwa upande wake Sure Boy ameonyesha uwezo mkubwa wa kupiga pasi ambazo zinafikia walengwa kwa usahihi na pia kuichezesha timu na kujenga mashambulizi.

Ingawa mara kwa mara na hata katika Kombe la Mapinduzi Sure Boy anachezeshwa katika nafasi ya kiungo, uwepo wa Feisal Salum, Yannick Bangala na Khalid Aucho wanaofanya vyema unaweza kulilazimisha benchi la ufundi la Yanga kumtumia pembeni katika nafasi ya Ntibazonkiza ambaye hata yeye hucheza kama kiungo wa kati au nyuma ya mshambuliaji.

Wakati Sure Boy na Nkane wakilipa kazi mpya benchi la ufundi la timu hiyo katika kuamua nani waanze katika kikosi cha kwanza kati yao na Ntibazonkiza au Moloko, mambo huenda yasiwe rahisi kwa kipa Abuutwalib Mshery aliyesajiliwa kutokea Mtibwa Sugar na Crispin Ngushi aliyenaswa akitokea Mbeya Kwanza.

Mshery ingawa amekuwa ndiye chaguo la kwanza kwa sasa, ana nafasi finyu ya kuendelea kuwa kipa namba moja mara baada ya kurejea kwa Djigui Diarra ambaye kwa sasa yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Mali kinachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) huko Cameroon.

Uzoefu, utulivu, uwezo mkubwa wa kuwasiliana na timu, kupanga safu ya ulinzi, kucheza mpira kwa miguu na kuondoa hatari za timu pinzani ni sifa ambazo zinampa fursa nzuri Diarra kuanza mbele ya Mshery.

Kwa upande wake Ngushi ana mlima mrefu wa kupanda ili kuweza kulishawishi benchi la ufundi la Yanga kumpa nafasi kutokana na uwepo wa nyota wanaofanya vizuri katika nafasi ya mshambuliaji wa kati.

Nyota huyo ambaye hadi anajiunga na Yanga alikuwa ameifungia Mbeya Kwanza mabao matatu, anakabiliwa na ushindani kutoka kwa straika tegemeo wa Yanga, Fiston Mayele ambaye ni miongoni mwa wafungaji bora wa Ligi Kuu hadi sasa akiwa na mabao matano, Heritier Makambo ambaye licha ya kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza, ameshafunga mabao matano kwenye michuano yote, matatu kwenye Kombe la Shirikisho la Azam na mawili kwenye Kombe la Mapinduzi pamoja na Yusuph Athuman.

Mwenyekiti wa kamati ya ufundi ya Yanga, Dominick Albinus ‘Baba Paroko’ alisema kuwa usajili wanaofanya ni wa malengo ya muda mrefu.

“Ni mpango wa muda mrefu ambao Yanga tumepanga kuwekeza kupitia kwa vijana wa Kitanzania ambao tunaamini watakuwa na mchango kwa timu yetu ya taifa pia siku za usoni. Wachezaji tuliowasajili ukiwatazama ni vijana wenye vipaji licha ya umri wao mdogo,” alisema Baba Paroko.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ramadhani Kampira alisema kuwa nyota wapya wa timu hiyo wanapawa kufanya kazi ya ziada ili kuchukua nafasi kikosini kwani waliopo tayari wameshamudu mazingira na mbinu za benchi la ufundi ambalo linawaamini.