Mnabishaa! Tukutane baadae

Muktasari:

YANGA na Namungo zinakiwasha jioni hii kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini hapa katika mechi ya Ligi Kuu, huku timu hizo zikiwa na rekodi ya aina yake.

YANGA na Namungo zinakiwasha jioni hii kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini hapa katika mechi ya Ligi Kuu, huku timu hizo zikiwa na rekodi ya aina yake.

Timu hizo hazijawahi kufungana kwenye mechi yoyote ya ligi katika mara zote tatu walizokutana, lakini safari hii kuna mkwara mzito umetoka kwenye mabenchi yote mawili kwamba; “lazima kieleweke”

Kocha wa Namungo, Hemed Moroco amesisitiza kwamba anajua Yanga itaingia kwa nguvu kwenye mechi kutokana na hamasa ya kocha mpya, lakini wao wamejipanga kimkakati. Ingawa habari za ndani zinadai kwamba mechi hiyo ndiyo iliyoshikilia kibarua cha Morocco na kwamba akipigwa tu baibai. Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesisitiza kuwa mechi hiyo ni ngumu lakini kwa walivyojipanga kuna dalili zote za pointi tatu. Rekodi ya mechi zilizopita kwenye ligi ziko hivi:


NAMUNGO 1-1 YANGA MACHI 15

Bao la Yanga lilifungwa na Tariq Seif, dakika ya 5 akiunganisha kwa kichwa krosi iliyochongwa kwa umaridadi na Juma Abdul.

Dakika ya 61, Bigirimana Blaise aliunganisha kichwa na kuipatia bao la kusawazisha Namungo na mpira kumalizika kwa bao 1-1.


YANGA 2-2 NAMUNGO JUNI 24

Dakika ya 51, Edward Manyama aliifungia Namungo bao la kuongoza kwa kichwa na dakika ya 69, akaongeza la pili akimpokonya mpira beki wa Yanga, Said Makapu wakati akiupaka rangi mpira na kufunga.

Yanga walianza mashambulizi na dakika ya 79, David Molinga ‘Falcao’ alifunga akimalizia krosi ya Haruna Niyonzima aliyeng’ara katika mchezo huo.

Dakika ya 90, Molinga tena aliifungia Yanga bao la pili akimalizia krosi ya Makapu.


YANGA 1-1 NAMUNGO NOVEMBA 22

Dakika ya 13, Carlos Carlinhos alitupia akiunganisha kwa kichwa krosi ya Kibwana Shomary

Iliwachukua dakika mbili tu Namungo wakarejesha bao dakika ya 15, Steven Sey na kumuacha Metacha Mnata akishangaa.

Mchezo huu huenda ungewapa Namungo ushindi baada ya dakika 90, Shiza Kichuya kuangushwa katika eneo la hatari na kupewa penalti, lakini Bigirimana alikosa mkwaju huo baada ya Metacha kupangua.


WACHEZAJI WA ZAMANI

Akizungumzia mchezo huo, mchezaji wa zamani Yanga, Edibily Lunyamila alisema: “Mpira mechi za mwisho sasa Namungo anahitaji matokeo kutokana na nafasi aliyopo sio salama kwake, huku Yanga akihitaji ubingwa, hii ni mechi ambayo kila mmoja anahitaji matokeo, lakini Namungo ndiye atakuwa na presha kubwa zaidi.”

Naye Ally Mayay ambaye ni staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars alisema: “Ni mechi ngumu sana kwa timu zote, Namungo ana presha kubwa, licha ya kuwa na wachezaji bora, lakini hawapati matokeo ila wachezaji wake wana uwezo kila moja ukimtizama anaweza kuamua matokeo.”

Mayay amesema ili Yanga washinde mchezo huo Kocha Mkuu wao, Nasreddine Nabi anatakiwa kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia morali waliyokuwa nayo kwenye mechi dhidi ya Simba waendelee nayo.


KOCHA NAMUNGO

Akizungumzia mtanange huo, Kocha Morroco wa Namungo amemtaja Nabi kuwa kikwazo. “Nabi ndiye atafanya mechi iwe ngumu, lakini hata hivyo tumejipanga kushinda na kuvuna pointi tatu, mechi yangu ya kwanza kama kocha mkuu ilikuwa dhidi ya Yanga tulitoka sare ya mabao 2-2 na ilikuwa tuishinde ile mechi, ile mechi ilinifunza jambo,” alisema Morocco licha ya kwamba viongozu wake walikwepa kuzungumzia tetesi za mechi hiyo kushikilia hatma ya ajira yake.

Alisema pamoja na kuwakosa wachezaji Stephen Sey, Blaise Bigirimana na Carlos Protas ambao ni majeruhi, lakini sio kigezo cha wao kutochukua pointi tatu.

“Kwa vyovyote vile tunahitaji pointi tatu ili kupanda kwenye msimamo.” Namungo ni ya 11 kwenye msimamo ikiwa na pointi 32 na Yanga ni ya pili na pointi 57.


YANGA KUKOSA hawa

Meneja wa Yanga, Hafidhi alisema wamejipanga kushinda kwa namna yoyote licha ya kuwakosa wachezaji kadhaa ambao ni majeruhi na wenye sababu binafsi.

Hafidhi alithibitisha nyota watano wa kikosi cha Yanga wameshindwa kusafiri kwenda Lindi kwenye mchezo dhidi ya Namungo kutokana na sababu mbalimbali.

Wachezaji hao ni Carlos Carlinhos, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Farid Mussa, Yassine Mustapha ambao ni majeruhi pamoja na Haruna Niyonzima mwenye matatizo ya kifamilia.

Katika orodha ya wachezaji hao watano waliobaki Dar es Saalam Carlinhos, Ninja na Mustapha wote wapo kikosi cha kwanza na kukosekana kwao maana yake nafasi zao zitazibwa na wengine.

Nafasi ya Carlinhos inaweza kuchezwa na Deus Kaseke au Zawadi Mauya ilhali nafasi ya Ninja wanaweza kucheza Lamine Moro, Dickson Job, Said Juma Makapu na Bakari Mwamnyeto. Ligi Kuu imekuwa na msisimko wa aina yake kila timu ikipambana kushinda.