Mmoja atemwa Mbeya City, Sabilo, Tariq wakiivaa Simba

Mbeya. Wakati Mbeya City ikishuka uwanjani dakika chache zijazo kuwavaa Simba, kocha mkuu wa timu hiyo, Mubiru Abdalah amemuondoa mchezaji mmoja, beki Eradius Salvatory kwenye kikosi kinachoanza.

Mbeya City haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo wakiambulia sare pekee na leo inahitaji kuwapa raha mashabiki ambao wamekosa mzuka kwa muda mrefu tangu waliposhinda Oktoba 25 dhidi ya Polisi Tanzania.

Katika kikosi alichoanzisha kocha huyo Mganda ni Lameck Kanyonga, Kenneth Kunambi, Brown Mwankemwa, Hassan Mohamoud, Juma Shemvuni, Hassan Nassoro, Richardson Ngy'ondya, George Sangija,Tariq Seif, Awadh Juma na Sixtus Sabilo.

Hata hivyo kombinesheni ya Seif, Awadh na Sabilo imekuwa na maelewano mazuri huku takribani mechi nne za nyuma wakifunga bao ukiachilia ile iliyomalizika kwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya Geita Gold.

Sabilo na Seif wamehusika katika mabao 11 ikiwamo asisti nane walizotengeneza wawili hao na kuifanya timu hiyo kuwa nafasi ya sita kwa pointi 18.

Sabilo pekee amefunga mabao saba na kusaidia sita, huku Seif akifunga manne na asisti mbili na leo wataiongoza City kumenyana na Simba.