Mkwara wa Ihefu kwa Yanga

WAKATI Yanga ikijivunia rekodi ya kucheza mechi 49 bila kupoteza, Ihefu imesema leo huenda ikawa timu ya kwanza kuwatibulia vigogo hao na kubaki na pointi tatu nyumbani.

Yanga imekuwa tishio Ligi Kuu baada ya kucheza dakika 4,410 bila kupoteza, ambapo leo Jumanne watakuwa kwenye Uwanja wa Higland Estate wilayani Mbarali kuwakabili Ihefu wanaochechemea mkiani.

Hadi sasa Yanga ndio inaongoza ligi kwa pointi 32 ikiwa haijapoteza mechi yoyote baada ya kushuka uwanjani mara 12 msimu huu, huku Ihefu wakiwa mkiani kwa pointi nane na michezo 13.

Yanga kabla ya leo msimu huu, iliichapa Ihefu ugenini mabao 3-0 (Desemba 23, 2020), marudiano Wanajangwani walishinda 2-0 (Julai 15, 2021), jambo ambalo mastaa watawajengea kujiamini zaidi.

Ihefu ambayo ilipanda msimu wa 2020/21 na kushuka uliofuata, kabla ya mchezo huo imecheza mechi 13, imeshinda miwili, sare mbili na imefungwa 9 na imejikusanyia pointi 8. Na huu tangu waanze kupanda msimu wa kwanza kabla ya kushuka utakuwa mchezo wao wa tatu kukuta.

Japokuwa ni mara chache kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, kubadilisha kikosi golini ni Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Joyce Lomalisa, Dickson Job na Yanick Bangala uwezekano wa kupangwa Bakari Mwamnyeto ni mdogo kutokana na kuumwa kwake.

Viungo ni Khalid Aucho, Gael Bigirimana, mawinga ni Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, straika wa mwisho ni Fiston Mayele kinara wa mabao wa ligi hiyo akifunga mabao 10.

Kikosi cha Ihefu, kinachocheza mara kwa mara chini ya kocha Juma Mwambusi, makipa wanabadilishana James Ssetuba/Shaban Kado, mabeki wa kati ni Lenny Kisu mkongwe Juma Nyoso, kulia yupo Wadada, kusho ni Mwasapili.

Viungo wapo Onditi, Papy Tshishimbi, ilhali mawinga ni Tegere na Joseph Mahundi.