Mkenya agundua mazito Yanga

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

SIRI imefichuka. Kumbe ile ishu ya Yanga kuruhusu mabao mepesi tatizo ni makipa wao kutokuwa fiti kwa kiwango kinachotakiwa.

SIRI imefichuka. Kumbe ile ishu ya Yanga kuruhusu mabao mepesi tatizo ni makipa wao kutokuwa fiti kwa kiwango kinachotakiwa.

Jambo hilo limebainishwa na kocha mpya wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa ambaye juzi alisaini rasmi mkataba wa kuanza kazi ndani ya Yanga akichukua nafasi ya Mrundi Vladimir Niyonkuru aliyetimuliwa mapema.

Kocha huyo mpya ametangulia kambini akianza kazi ya kibabe kwa dozi ya kutwa mara mbili lakini alipowaona wachezaji wake wawili tu akasema “kwa staili hii ilikuwa lazima Yanga ipigwe mabao mengi.”

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kusaini mkataba, Ssiwa alisema katika siku tatu tu ambazo alikuwa kambini sambamba na makipa wawili Farouk Shikhalo na Ramadhan Kabwili ameshtuka kwamba kiwango cha kuwa fiti kilikuwa chini sana.

Ssiwa alisema katika mazoezi yake ya kwanza aliona kwamba makipa hao wako fiti kwa asilimia 45 hali ambayo ingekuwa ngumu kuwa na msaada ambao Yanga iliutarajia.

“Bahati nzuri ligi imesimama lakini kwa asilimia hizo ni vigumu sana kipa kuweza kuisaidia timu kubwa kama Yanga kama ambavyo wengi wanatarajia,” alisema Ssiwa.

“Sina shaka na ubora kwa maana ya vipaji vyao, hawa ni makipa bora sana, lakini kipa ili uwe bora zaidi ni lazima uwe fiti kwa sababu ukiwa fiti unaweza kufanya uamuzi wowote mgumu katika mchezo.”

Siwa alisema baada ya tathmini hiyo, sasa ni kazi moja tu kuwaimarisha makipa hao huku akimsubiri Metacha Mnata ambaye alikuwa katika majukumu ya kikosi cha Taifa Stars.

Mkenya huyo alisema anahitaji siku zisizopungua 17 kwa makipa wake kuanza kuonyesha ubora ambao mashabiki wa Yanga wanausubiri.

“Unajua uzuri nilikuwa nafuatilia sana mechi za Yanga, sidhani kama kuna mechi nimewahi kuikosa kuangalia, najua makosa ya hawa makipa wote walipokuwa wanacheza.

“Nimewaambia huu ni wakati wa kazi kwa asubuhi na mchana, hakuna kupumzika, najua watakuwa katika wakati mgumu lakini kama mnavyofahamu Yanga ni klabu yenye presha kubwa, naijua, kwahiyo lazima tukimbie kutafuta mafanikio.

“Ukiacha hawa wanaocheza lakini pia kuna kazi ya kumuimarisha Kabwili, ni kipa mdogo na mwenye kipaji kikubwa, tunatakiwa kumuimarisha ili naye acheze, yupo hapa kama sehemu ya timu.”


Akikubali kikosi

Yanga inafanya mazoezi na wachezaji 16 tu kambini na Ssiwa amewaangalia wanaofanya mazoezi sasa na kusema kikosi hicho kina watu bora ambao kama wataunganishwa vizuri kuna kitu watavuna msimu huu.

“Nimemkuta kocha wangu Mwambusi (Juma) hapa kambini na niseme amewaimarisha sana vijana katika maeneo mengi, niliona kuna mambo yanapungua katika mechi za hivi karibuni, bahati nzuri Mwambusi amewaimarisha hawa waliopo.

“Mimi naamini kama hawa wengine watarejea haraka na wakaunganishwa vyema Yanga ina kikosi imara sana ambacho kinaweza kufanya mambo mazuri msimu huu.”