Mkenya aachiwa msala wa Msuva

MSHAMBULIAJI wa Harambee Stars, Masoud Juma amebeba matumaini ya mashabiki wa Difaa El Jadida ambao wanaamini Mkenya huyo anaweza kuziba pengo la Mtanzania, Simon Msuva ambaye aliiichezea timu hiyo kwa mafanikio kabla ya kujiunga na Wydad Casablanca.

Juma, 25, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Bandari, SoNy Sugar na Kariobangi Sharks za Ligi Kuu Kenya, ameanza kuonyesha makali yake akiwa na Difaa El Jadida ambayo ipo kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kupitia ukurasa rasmi wa mtandao wa kijamii wa facebook wa chama hilo la zamani la Msuva, mashabiki walitumia uwanja wa kutoa maoni yao kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Rapide Oued Zem kwa kusema wazi Mkenya huyo ndiye mrithi sahihi wa Msuva ambaye bado anaendelea kutesa kwenye Ligi hiyo.

Miongoni mwa mashabiki hao, Ashiraf Cherif alisema, “Tulikuwa na shida kwenye safu yetu ya ushambuliaji lakini kwa sasa naona kuna mwanga, hizi ni dalili nzuri ambazo amezionyesha Juma, naamini anaweza kuongeza nguvu ambayo ilipungua baada ya kumpoteza Msuva.”

Katika mchezo huo, Juma alitupia bao moja ambalo lilichangia chama hilo kuvuna pointi tatu ambazo zimewasaidia kujioandoa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Kwa upande wake Msuva amefurahishwa na habari za Mkenya huyo, anaamini anaweza kuwa shujaa mpya ndani ya klabu hiyo ambayo ilimfanya Wamarocco wamtambue hadi kupata shavu la kujiunga na miamba ya soka nchini humo, Wydad Casablanca.

“Nilikuwa nikiumia kila nikicheki msimamo na kuona timu ipo kwenye hatari ya kushuka daraja, siwezi hata siku moja kufurahi kuona wakiwa kwenye wakati mgumu kiasi kile, nashukuru Mungu wamesimama kwa sasa na wanaendelea vizuri kama mwanzo tu,” alisema.

Wydad Casablanca ambao jana, Jumapili walikuwa na mchezo wa kiporo cha Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ndio vinara wa Ligi Kuu Morocco, wanaongoza msimamo wa Batola Pro wakiwa na pointi 18.