Miquissone: Ubingwa wa VPL nyie chongeni

Muktasari:

Luis anasema Yanga waliweka ofa nono kuliko Simba katika kuiwania saini yake, lakini akachagua kwenda Msimbazi.

KATIKA toleo lililopita Luis Miquissone alielezea dili lake na klabu za Uarabuni, lakini akahitimisha kwamba Simba ndiyo yenye uamuzi wa kumuuza au kutomuuza kwavile ana mkataba mrefu nao.

Katika muendelezo wa leo Luis anaanza na ishu yake na Yanga;

Simba baada ya kucheza mechi ya kwanza na UD Songo ugenini Msumbiji, kilifanya kikao na Luis ambaye alieleza kuhusu masuala yake yote ya kimkataba ili kupatikana.

Baada ya hapo Simba hawakuendelea kwa spidi ya kumtaka. Kumbe Yanga pia walikuwa wakimhitaji na wakaingia kikamilifu ili kumnasa winga huyo ambaye alionyesha kiwango bora zaidi katika mechi ya marudiano na Wekundu wa Msimbazi iliyopigwa Dar es Salaam.

Simba wakastukia mchongo kwamba Luis anatakiwa na Yanga, ambao walifikia hatua ya kujiamini kwamba watainasa saini yake. Jambo hilo liliwastua Simba. Mara hii Wekundu wa Msimbazi wakarudi kwake kwa nguvu kubwa zaidi.

Yanga walipotuma wawakilishi wao Msumbiji alikokuwa anaishi Luis, wakaambulia patupu kwa sababu Simba walishamtorosha.

Luis anasema baada ya Simba kujua Yanga wapo Msumbiji walimtumia tiketi ya ndege mpaka Afrika Kusini, akaenda huko.

“Baada ya kufika Afrika Kusini Yanga walikuwa wananipigia simu ambazo sikupokea kwani nilikuwa tayari nimekutana na kiongozi mmoja wa Simba,” anasema.

“Kiongozi huyo hakutaka kabisa niongee na Yanga kwani tulifanya mazungumzo ya kuhusu kusaini mkataba yaliyochukua muda mrefu lakini mwisho wa siku tulikubaliana nikasaini,” anasema.

“Dili la Yanga lilikufa hapo hapo na ilibidi niwaambie ukweli ingawa hawakupenda kwani waliamini wangeweza kunipata kwa kuwa waliweka pesa nyingi kuliko zile za Simba.

“Nilifanya uchunguzi na nikatumia taarifa nilizopata. Simba ilikuwa chaguo sahihi kwangu kuliko Yanga ambao waliweka pesa nyingi na hilo naliona wakati huu na sijutii uamuzi niliofanya,” anasema Luis ambaye anabainisha kuwa kule Mamelodi Sundowns alikokuwa amepelekwa kwa mkopo aliondoka kiroho safi kwavile waliamini alikuwa hajaiva.

BAO LA AHLY

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Ahly ambalo lilifungwa na Luis ambaye alichaguliwa katika wachezaji waliongia katika kikosi cha wiki wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na bao lake likachaguliwa kuwa bora.

“Hii imenipa hamasa na morali ya kushindana zaidi katika mashindano haya ili kuisaidia timu yangu kufanya vizuri na kufikia malengo ambayo wamejipangia,” anasema.

“Bao lile lilikuwa bora zaidi ya zawadi ambayo wameitoa CAF kwani liliisaidia timu kupata pointi tatu ambazo tulikuwa tunahitaji na limeongeza wasifu wangu wa kufuatiliwa na timu nyingine zaidi,” anasema Luis.

KUHUSU MOSIMANE

Luis aliondoka kwa mkopo katika kikosi cha Mamelodi Sundowns wakati huo kocha alikuwa, Pitso Mosimane ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Al Ahly ya Misri.

Luis anasema wala hana tofauti na kocha huyo mkubwa Afrika ndio maana kabla ya timu yake kucheza na Simba alimtaja kama moja ya wachezaji hatari na wa kumtazama.

“Ambacho nilipanga kufanya katika mechi ile ni kumuonyesha nimezidi kuimarika na kuwa bora tofauti na wakati nipo chini yake, nilitaka kumuonyesha kuwa kile ambacho alikisema kabla ya mechi hakuwa amekosea ndio maana nilipambana ili kuisaidia timu yangu na mpaka nikafunga bao.

“Namuheshimu Pitso ni moja ya makocha wakubwa hapa Afrika licha ya kufanya uamuzi wa kuniacha wakati ule, niliamini kuna wakati tunaweza kukutana tena kwani maisha ya mpira yanazunguka,” anasema.

MECHI YA DABI

Mechi ya Ligi Kuu iliyopita ya Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1, ilimpa lawama Luis akituhumiwa kucheza chini ya kiwango yeye pamoja na staa Clatous Chama.

Lakini Luis anasema ishu ni presha ya mechi tu. “Mechi yoyote lazima uwe na presha kama mchezaji lakini mara nyingi kwenye mchezo huu unakuwa tofauti kwani wachezaji tunacheza kwa nafasi kwa kila mmoja kuonyesha kiwango chake,” anasema.

“Tangu nilipotoka nilikuwa nakutana na presha kama hii ya mechi kubwa kwahiyo nimezoea na inapofika huwa natamani kuicheza kwa kuamini naenda kuonyesha jambo bora la kuisaidia timu yangu.”

Luis amewahi kufunga bao moja katika mechi moja dhidi ya Yanga ambayo ilikuwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), timu yake ilipoondoka na ushindi wa bao 4-1.

UBINGWA ACHENI WACHONGE

Luis anasema kutokana msimamo wa ligi ulivyo kama watafanikiwa kufanya vizuri katika mechi zao wanaweza kuwa vinara wa msimamo na itakuwa ngumu kushuka tena.

“Ukiangalia timu yetu ni nzuri ambayo inaweza kutetea ubingwa wa ligi bila ubishi ila kwa kuwa ligi ni mashindano tunaendelea kushindana mpaka mwisho na kuona kile ambacho tutakipata,” anasema.

“Kama tukicheza katika ubora kama huu tuliokuwa nao wakati kwenye mechi zetu za ligi tunaweza kutetea ubingwa mapema kabla ya kucheza mechi za mwisho.

“Kikubwa tunaendelea kupambana kama wachezaji wote wa Simba na tumedhamiria kuchukua ubingwa huu wa ligi kwani ndio malengo yetu ambayo tumejipangia,” anasema Luis na kuongeza kuwa anawakubali sana mashabiki wa Simba.

“Najisikia raha sana ninapocheza mbele ya mashabiki wengi haswa hawa wa Simba ambao huwa wananipa hamasa ya kujituma na kucheza zaidi ya nilivyojiandaa siku hiyo,” anasema.

“Niwaambie mashabiki wa Simba natambua mchango wao muda wote ninapowaona katika kiwanja na natamani kufanya kile ambacho wanahitaji.

“Kuna wakati natambua nguvu yao kwani ukiachana na pale uwanjani huko mtaani nikikutana nao huwa wananipa nguvu kama kuja kwa wingi nilipo, kunisaidia nilipokwama na mambo mengine.”

KUACHA HISTORIA

Luis anasema anatambua kuwa mambo aliyofanya na aliyodhamiria kuifanyia klabu hiyo ni wazi yatazivutia klabu nyingine lakini amesisitiza kabla ya kufanya uamuzi ya kuondoka katika kikosi cha Simba anataka kuweka historia na alama ili aweze kukumbukwa kwa muda mrefu.

“Unajua Simba ni moja ya timu kubwa kwa sasa hapa Afrika na hakuna mchezaji ambaye hatamani kuitumikia timu hii ambayo na kiu ya mafanikio,” anasema.

“Nataka kufanya makubwa ili muda wangu ukifika mwisho hapa Simba niache alama na ikitokea hata wakati mwingine nataka kurudi Simba iwe rahisi kutokana na yale ambayo nitakuwa nimeyafanya,” anaongeza Luis.