Mifumo mitano kumbeba Chikwende Simba, kuwachomoa watano

KIUNGO Mshambuliaji mpya wa Simba, Perfect Chikwende aliyesajiliwa kutokea FC Platinum ya Zimbabwe kama atapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza anakwenda kuingia katika mifumo mitano tofauti.

Usajili huo wa Chikwende mbali ya kuingia katika mifumo mitatu tofauti anakwenda kuhatarisha nafasi ya kucheza kwa nyota watano ambao walikuwa wanatumika mara kwa mara katika kikosi cha kwanza au kuingia kipindi cha pili kabla ya usajili wake.

fumo wa kwanza ambao Chikwende utampa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza (4-3-3) na hapa atatumika katika nafasi ya washambuliaji watatu ambao wanaweza kuwa pamoja na John Bocco, Clatous Chama, huku katika eneo la viungo watatu watakuwepo, Luis Miquissone, Larry Bwalya na Jonas Mkude.

Katika mfumo huu Chikwende atakuwa akicheza kutokea pembeni kulia na jukumu lake la kwanza litakuwa kutengeneza nafasi za kufunga kwa washambuliaji au kufunga mwenyewe kama ilivyokuwa katika mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, uwezo wake wa kukimbia kwa spidi kali hautakuwa rafiki kwa mabeki wavivu kwani atakuwa akiwasumbua mara kwa mara.

Chikwende anaweza kuingia katika mfumo mwengine wa (4-2-3-1), ambao atacheza katika eneo la viungo watatu washambuliaji akiwa pamoja na Chama, Miquissone wakati nyuma yao watakuwepo viungo wawili wakabaji Mkude na Lwanga huku straika mmoja anaweza kucheza Meddie Kagere.

Katika mfumo huu Chikwende atacheza akitokea kushoto wakati na upande wa kulia atakuwepo Miquissone huku katikati yao atakuwa Chama ambaye jukumu lake litakuwa kuchukua mipira kwa viungo wawili wakabaji na kuwapelekea mawinga hao.

Chikwende na Miquissone watakuwa wanacheza kwa kufanana kukimbia na mipira katika boksi la wapinzani, kuwapiga vyenga mabeki, kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wengine, kufunga wenyewe endapo watapata nafasi hiyo na kutafuta faulo au penati za mara kwa mara ambazo zitakuwa na faida kwao.

Mfumo wa tatu ambao Chikwende anaweza kuingia ni (4-4-2), ambao huu atacheza nyuma ya straika ambaye anaweza kuwa Chriss Mugalu huku nyuma yao katika viungo wawili ambao ni Mkude na Bwalya na mawinga wawili Chama na Miquissone.

Chikwende faida ambayo atakuwa nayo hapa ni uwezo wake wa kufunga, kukimbia kwa spidi kwa kuwasumbua mabeki lakini anafaida ya kutengeneza nafasi za kufunga kwa wachezaji wenzake kama alivyofanya katika mechi ya marudiano na Simba akiwa FC Platinum ila wenzake walishindwa kuzitumia kwa kufunga mabao.

Mfumo wa nne ambao Chikwende anaweza kupata nafasi ya kucheza ni (3-5-2), na hapa takuwa katika eneo la viungo watano ambao anaweza kucheza sambamba na Mkude, Lwanga, Chama na Miquissone huku mbele yao wanaweza kuwepo mastraika wawili, Bocco, Kagere au Mugalu.

Majukumu ya hapa kwa Chikwende hayatakuwa yakitofautiana na yale ambayo atayafanya katika mifumo mingine mitatu ya mwanzo, kama kusaidia kukaba, kutengeneza nafasi za kufunga na kufunga mwenyewe.

Mfumo wa tano ambao anaweza kufiti kama Simba watakwenda kucheza kwaa kujilinda katika mchezo fulani kwa kutumia (4-5-1), Chikwende anaweza kucheza katika eneo la straika mmoja ambapo atasimama katikaa eneo la kushambulia akiwa mwenyewe.

Chikwende anauwezo wa kumiliki mpira na mgumu kupoteza akiwa nao mguuni kwake kwa maana hiyo akianza kama straika mwenyewe atakuwa akikaa na mpira kusubiri wenzake waliokuwa nyuma kujilinda zaidi kuja kumsaidia na atakuwa akiwapa pasi zilizokuwa sahihi.

Mara nyingi kwa timu yenye kupenda kushambulia kama Simba ni nadra kutumia mfumo wa namna hii ila kuna mechi kama dhidi ya Esperence de Tunis tena ugenini zinahitaji kujilinda zaidi ili kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa au kupata aina ya matokeo ambayo watahitaji na kama wakicheza tofauti na hivyo wanaweza kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.

Ukiachana na mifumo hiyo mitano ambayo inaweza kumbeba Chikwende katika kikosi cha kwanza kama akiwa fiti, kuna nyota wengine watano watakuwa na wakati mgumu wa kutumika mara kwa mara pengine kabla ya usajili wake kukamilika.

Nyota hao watakuwa na wakati mgumu wa kucheza kutokana wanatumika nafasi moja na Chikwende ambaye ukiangalia video zake mbalimbali pamoja na mechi mbili za Simba ni bora katika kufunga mwenyewe, kutengeneza nafasi za kufunga, kuwasumbua mabeki, anakimbia zaidi, aina yake ya uchezaji itakuwa ikifanana na Miquissone ni usajili mpya ambao utapewa nafasi zaidi.

Wachezaji hao watano ambao watakuwa katika wakati mgumu kupata nafasi ya kucheza mbele ya Chikwende ni Francis Kahata, Bernard Morrison, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Miraji Athumani na Said Ndemla ambaye muda mwingine huwa anacheza kama namba kumi.

Usajili huo wa Chikwende unaelezwa umekwenda kumchomoa Kahata katika usajili wa wachezaji wa mashindano ya ndani na atakuwa akitumika katika Ligi ya Mabingwa Afrika tu wakati mwenzake atacheza katika mashindano yote.

Maamuzi hayo yalifikiwa baada ya Kahata kugoma kutolewa kwa mkopo kwa kutaka Simba wavunje mkataba wake wa miezi sita uliobaki na wamlipe mkwanja wake au aendelee kukaa mpaka mwisho wa msimu mkataba wake utakapomalizika na hapo ataangalia mahala pengine kwa kwenda kucheza.

Kahata, Morrison, Ajibu na Miraji hata kabla ya kusajiliwa kwa Chikwende katika mzunguko wa kwanza walikuwa hawana nafasi katika kikosi cha kwanza na kutumika mara kwa mara kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wachezaji kama, Pascal Wawa, Joash Onyango, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na wengineo.

WASIKIE HAWA

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Alex Kashasha anasema kuna utamaduni ambao umejengeka kwa klabu kubwa za hapa nchini kumuona mchezaji fulani katika mechi moja akicheza vizuri ikiwemo kuwafunga hapo hapo wanamsajili na baadaye yanakuja kutokea masuala mengine ikiwemo kucheza chini ya kiwango.

“Kuingia huko kwa Chikwende katika kikosi cha kwanza akitokea kulia ni wazi Dilunga nafasi yake inaweza kuwa finyu ya kutumika mara kwa mara pengine kama ilivyokuwa kabla ya usajili huu kufanyika,” anasema.

“Lakini kwa ambavyo nimemuona Chikwende katika mechi mbili dhidi ya Simba akikutana na mabeki wenye kuweza kutumia zaidi ngumu na wagumu anakuwa rahisi kukabika na si msumbufu tena sidhani kama Simba wameliangalia hili kwani naamini si mchezaji wa daraja kubwa hivyo kama anavyotajwa na watu wengi,” anasema Kashasha.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema mpaka Simba wamefikia uamuzi ya kumsajili basi kuna vitu vya kiufundi ambavyo wameviona kutoka kwake.

Mwakingwe anasema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola ambaye wamekuwa wakishaurina jinsi ya kuitengeneza timu hiyo kuwa bora na miongoni mwa eneo hilo ni jinsi ambavyo wanatakiwa kusajili wachezaji bora.

“Simba wanatakiwa kuangalia zaidi mahitaji ya mashindano ya kimataifa kwani wanakwenda kukutana na wachezaji wa ukweli ambao nao wanatakiwa kuwa nao katika kikosi chao ili kushindana nao na kama ikiwa tofauti na hivyo hawataweza kufanya vizuri kwa maana hiyo naimani na kila usajili utaleta faida,” anasema Ulimboka.