Mibao ya Kagere yamkolea Pablo, nahodha Yanga afunguka

MABAO mawili aliyofunga straika wa Simba, Meddie Kagere dhidi ya Ruvu Shooting wakati Wekundu wa Msimbazi wakiizamisha Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 yamemfanya mkali huyo kukabiribia kuandika rekodi mpya kwa wageni nchini, huku Kocha Pablo Franco akiyakubali.

Pablo licha ya kutozungumza moja kwa moja, lakini kila straika huyo alipokuwa akiyaweka kimiani, alionekana kupiga makofi akiwa na furaha, sawa na ilivyokuwa kwa bao la tatu lililofungwa na Kibu Denis.

Kama hujui ni, Kagere aliyesajiliwa Simba mwaka 2018, huu ni msimu wake wa nne kucheza Ligi Kuu Bara na mabao mawili ya juzi yamemfanya afikishe jumla ya mabao 62, ikiwa ni 11 pungufu ya yale aliyofunga Amissi Tambwe ndani ya misimu yake sita katika ligi hiyo akiwa kinara.

Tambwe aliyeng’ara Simba na Yanga kabla ya sasa kuliamsha DTB inayoshiriki Championship (zamani Daraja la Kwanza) ndiye nyota wa kigeni aliyefunga mabao mengi katika ligi akitumia 73.

Hata hivyo, Kagere anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika Ligi Kuu Bara kutetea tuzo ya Mfungaji Bora akifanya hivyo 2018-2019 na 2019-2020, kama ataendeleza moto msimu huu kwa mechi zilizosalia anaweza kumpiku Tambwe na kuweka rekodi mpya.

Kagere aliyesajiliwa kutika Gor Mahia, mabao yake ya juzi yaliifanya Simba kufikisha pointi 14, lakini akifikisha mabao manne akimfikia Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania, huku akishikilia rekodi kwa sasa ndani ya Simba kuikusanyia Simba pointi nyingi msimu huu.

Kagere alifunga dhidi ya Dodoma Jiji, Namungo na juzi Ruvu ikiwa na maana mabao yake yameipa Simba jumla ya pointi tisa, huku alama nyingine tano zikichangiwa na wenzake ikiwamo penalti ya Rally Bwalya dhidi ya Polisi Tanzania. Mechi nyingine mbili Simba ilitoka sare.

Katika msimu wake wa kwanza, Kagere alifunga mabao 23 na kubeba tuzo aliyoitetea katika msimu wa pili akifunga 22 na msimu uliopita alitupia kambani mabao 13 na ukijumlisha na manne ya sasa imemfanya awe na mabao 62, mbali na mengine aliyoifungia timu hiyo katika mechi nyingine za mashindano zikiwamo za CAF, Kombe ASFC, Mapinduzi, SportPesa, Ngao ya Jamii na Kagame.

Tambwe katika misimu yake sita akicheza Ligi Kuu alianza kwa kufunga mabao 19 akiwa Simba na kubeba tuzo, kisha kufunga moja kabla ya kuhamia Yanga na kufunga mengine 14 na kumaliza msimu na mabao 14 na msimu wa tatu alitupia 21 akiweka rekodi ya mchezaji wa kwanza wa kigeni kuvuka mabao 20 na kutwaa tuzo.

Msimu wa nne alifunga mabao 11 kisha msimu wa tano kutoka kapa kwa vile alikuwa majeruhi na kumalizia msimu wa mwisho na mabao nane.

Kagere alisema amefurahishwa na kutunzwa kwa kumbukumbu hiyo itakayomfanya aongeze kasi ya ufungaji mabao kila mechi atakayocheza.

Alisema akiwa anafunga mabao mengi kila mechi atakapopata nafasi ya kufanya hivyo jambo la kwanza atakuwa anatimiza majukumu ya nafasi yake, kuisaidia timu pamoja na kuweka rekodi nyingine za namna hiyo.

“Malengo yangu ni makubwa mno kuisaidia timu kufikia kile ambacho tulijipangia mwanzo wa msimu ndio maana kila ukiona uwanjani napenda kujituma zaidi ya mechi iliyopita pengine ndio maana kila siku tunafanikiwa kama timu,” alisema Kagere na kuongeza;

“Ndio kwanza tupo katika mzunguko wa sita kikosi chetu kinazidi kuimarika kutokana na mabadiliko ila nitazidi kumwomba Mungu kila nikipata nafasi ya kucheza kutimiza majukumu yangu na kufunga mabao zaidi na kutoa mchango kwa wengine kama nitakutana na changamoto nyingine yoyote nipo tayari kukabiliana nayo.”


NAHODHA YANGA

Nahodha wa zamani wa Yanga, Fredy Mbuna alimchambua Kagere dhidi ya Tambwe na kusema straika huyo wa Simba ni mchezaji anayependa kujishughulisha uwanjani na kutafuta mipira ili afunge tofauti na Tambwe ambaye huwa anakaa sehemu moja.

Mbuna alisema Kagere si mzuri tu anapokuwa na mpira bali yupo fiti zaidi, ila Tambwe ananyumbulika japo kwake wote ni wazuri kwa kufunga mabao.

“Niwambie Simba wanapenda kujipa tabu wenyewe, kikosi chao kilivyo wanamhitaji Kagere zaidi kwani ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao hata katika mazingira magumu kama lile la Namungo,” alisema Mbuna na kuongeza;

“Kwa kasi aliyonayo Kagere naona rekodi ya Tambwe ataifikisha na kuivuka kabla hata ya misimu sita kufika kwani anajua mno kupachika mabao.”