Miasisti ya Chama funika bovu

CLATOUS Chama ni zaidi ya balaa, kwani rekodi aliyoiweka hadi sasa Ligi Kuu kama kiungo, inasisimua.

Kwani kabla hata msimu haujafikia tamati, Mzambia huyo tayari amevunja rekodi yake mwenyewe ya msimu uliopita wa mabao pamoja na kuasisti.

Msimu huu Simba ikiwa imesaliwa na mechi tisa kabla ligi haijamalizika, tayari Chama ameifungia timu yake mabao saba na kuasisti mara 13 na kuisaidia timu yake kuwa kinara wa mabao kwa sasa ikiwa na 58 katika mechi 25.

Kwa msimu uliopita, Mzambia huyo aliifungia Simba mabao mawili na kuasisti mara 10 tu, hivyo kwa rekodi za sasa jamaa katisha mbaya na kuifukuzia rekodi iliyowahi kuwekwa na Ibrahim Ajibu alipokuwa Yanga misimu miwili iliyopita alipofunga mabao saba na kuasisti mabao 15.

Rekodi za ssa zinaonyesha Chama anashikilia nafasi ya kwanza kwa walioasisti mara nyingi na kuna baadhi ya nyota wa Simba wamenufaika zaidi na pasi hizo za upendo kutoka kwa Mzambia huyo.

Walionufaika na asisti za Chama ni, Luis Miquissone, Chriss Mugalu na Meddie Kagere ambaye kila mmoja amepokea pasi tatu.

Wa kwanza kupokea pasi ya mwisho kutoka kwa Chama ilikuwa katika mechi ya ufunguzi wa msimu ambayo Simba walicheza dhidi ya Ihefu alitoa pasi ya mwisho ambayo Mzamiru Yassin alikwenda kufunga bao la pili dakika 42.

Alitoa pasi ya mwisho tamu, kali tena ya kuvutia kwa kisigino iliyokwenda kumkuta, Chriss Mugalu aliyefunga bao lake la kwanza msimu huu katika mechi ya ligi dhidi ya Biashara United waliolala kwa mabao 4-0.

Chama alitoa pasi ya mwisho katika mechi ya JKT Tanzania iliyochezwa katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambayo, Meddie Kagere aliitumia kwa kufunga bao la tatu katika mechi hiyo, huku pia akimpsia Hassan Dilunga wakati wakiiangamiza Coastal Union kwa mabao 7-0 jijini Arusha.

Oktoba 31, Chama alitoa pasi ya mwisho kwa kifua iliyokwenda kumkuta Bocco na kufunga bao lake la kwanza katika mechi dhidi ya Mwadui ambao walifungwa mabao 5-0.

Mchezo uliofuata Simba walikuwa nyumbani Uwanja wa Uhuru dhidi ya Kagera Sugar na walishinda mabao 2-0, Chama alitoa pasi ya mwisho katika bao la pili ambalo alifunga Said Ndemla.

Desemba 13, mwaka jana Simba walipata ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Sokoine Mbeya na bao lao lilifungwa na Bocco ambaye alipokea pasi ya mwisho kutoka kwa Chama dakika 32.

Katika mechi ya marudiano dhidi ya Ihefu ambayo Simba walishinda mabao 4-0, Chama alitoa pasi za mwisho mbili ya kwanza ilikuwa dakika 39 kwa Kagere aliyefunga bao la tatu na lile la nne lililofungwa na Mugalu dakika 84.

Kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Mtibwa Sugar huku Chama akitoa pasi ya mwisho kwa kisigino aliyokwenda kumkuta, Luis aliyefunga bao la tano kabla ya kumpa tena Luis kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba waliposhinda 2-0.

Mechi ya mwisho ya ligi Simba walipoifunga, Dodoma Jiji 3-1, Chama tena alitisha kwa kutoa pasi mbili za mwisho ya kwanza ikiwa kwa Luis na nyingine kwa Mugalu.


MSIKIE CHAMA

Mwanaspoti lilipomtafuta Chama anasema anapokuwa uwanjani huwa anafikiria kucheza katika kiwango bora ili kuisaidia timu yake kufikia mafanikio ya kushinda kila mechi.

“Hizo rekodi nyingine huwa zinakuja tu kutokana na malengo yangu ambayo nimejiwekea lakini kuhusu kufunga ujue mimi ndio nakuwa mchezaji wa mwisho kufunga ila kuna kazi kubwa ambayo imefanywa na wenzangu,” alisema Chama na kuongezea;

“Kikubwa ni ushirikiano katika kikosi hicho cha Simba kwa kila mchezaji kuonyesha uwezo ambao anao kwenye kutimiza majukumu yake.”

Naye kocha wa Simba, Didier Gomes alisema miongoni mwa viongo bora waliokuwa hapa nchini pamoja na mashindano mengine hata acha kumtaja Chama kutokana na ubora wake.

“Amekuwa na mchango katika timu ndio maana ameweka rekodi kama hizo za kutoa pasi za mwisho nyingi pamoja na kufunga mabao muhimu lakini haya yote asingeweza mwenyewe bila ya kushirikiana na wenzake,” alisema Gomes.