Mhilu ataka kumpindua Kagere

Friday November 20 2020
kagere pic

Straika wa Kagera Sugar, Yusuph Mhilu amesema anataka kufunga mabao zaidi ya 13 aliyofunga msimu ulioisha, huku akiweka wazi kutamani kuvunja  rekodi ya mshambuliaji wa Simba,Meddie Kagere.

Misimu miwili aliyocheza Kagere, Ligi Kuu Tanzania Bara amechukua kiatu cha dhahabu mara mbili, msimu wa 2018/19 alipofunga mabao 23 na msimu uliopita alipachika nyavuni mabao 22.

Mhilu ambaye katika raundi 10 za mechi za ligi msimu huu amefunga mabao manne mpaka sasa ameiambia Mwanaspoti Online kuwa anatamani kuwa mtetezi wa wazawa kwa kuchukua kiatu cha dhahabu ambacho kipo kwenye utawala wa Kagere.

"Lazima nikubali kwamba Kagere ni mpambanaji.Ukitaka kumshinda mpinzani wako ujue ubora wake na udhaifu wake, hivyo vyote nimevisoma kwa Kagere nipo tayari kwa mapambano hayo,".  

"Silaha yangu ya kufikia mafanikio hayo ni kuongeza bidii ya mazoezi, nidhamu ya kazi ikiwemo kulana kuupumzisha mwili kwa wakati.Naamini naweza nikaigeuza ndoto kutoka kwenye maono kuja kwenye vitendo,"amesema Mhilu.

Pamoja na ndoto zake hizo amezungumzia ugumu wa ligi na namna timu zinavyotaka kujiweka kwenye mazingira ya kutoshuka daraja mapema kwamba kunamuweka kwenye kiwango muda wote, ili awe msaada kwa timu yake.

Advertisement

"Ugumu wa ligi nimeuchukulia kama nafasi kwangu ya kufanya bidii zaidi, hilo ndilo litanifanya nifikie malengo yangu ya msimu huu,"amesema.

_________________________________________________________

 By OLIPA ASSA


Advertisement