Mghana aitanguliza Namungo kimataifa

Mghana aitanguliza Namungo kimataifa

Muktasari:

Namungo ilikata tiketi ya ushiriki wa michuano hii ya kimataifa baada ya kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC), licha ya kupoteza mabao 2-0 mbele ya Simba ambayo tayari ilishakuwa na tiketi ya ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwani ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

MSHAMBULIAJI Mghana, Steven Sey amekuwa mchezaji wa kwanza kwa timu za Tanzania kufunga bao kwenye michuano ya Afrika kwa msimu huu, baada ya kuitanguliza timu yake ya Namungo mbele ya Al Rabita ya Sudan Kusini katika merchi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Sey amefunga mara mbili kwenye Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Wasudan Kusini na kuwapa raha mashabiki waliojitokeza kwenye uwanja huo kuishuhudia Namungo ikitupa karata yake kwa mara ya kwanza ya ushiriki wake wa michuano hiyo ya kimataifa.

Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa msimu huu na 'Southern Killers' kutoka Singida United alifunga bao la kwanza dakika ya 20 na 39 na kuiweka kwenye nafasi nzuri Namungo ikienda mapumziko.

Namungo inayonolewa kwa sasa na Hemed Suleiman 'Morocco' aliyechukua nafasi ya Mrundi, Thiery Hitimana, wameonyesha kiwango cha hali juu mbele ya Al Rabita ambayo ni timu ya Daraja la Pili nchini kwao na kuwazidi ndani ya dakika hizo 45 za kwanza.

Katika kipindi hicho cha kwanza Namungo walikuwa na nafasi ya kufunga zaidi ya mabao hayo, kwani wapinzani wao walionekana kuchoka haraka na kuishia kumlalamikia mwamuzi kila mara na hata bao la pili la Namungo walililalamikia wakidhani Sey aliotea kabla ya kufunga.