Mechi ya Kagere, Bocco

LEO ni siku ya 271 tangu mwaka huu uanze. Simba inaanza rasmi safari ya kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Bara ikiwa na rekodi nzuri mkononi dhidi ya Biashara United lakini kwa mujibu wa rekodi ni mechi ya Kagere na Bocco.

Katika mechi sita walizokutana tangu msimu wa 2018-19, Mnyama kashinda tano, kutoka sare moja na hawajapoteza hata mmoja.

Meddie Kagere ameifunga Biashara mabao matatu kati ya 12, kama ambavyo ilivyo kwa John Bocco aliyewafunga mabao mawili kutokana na uwezo wao wa kuifunga timu hiyo huenda wakaendeleza moto huo kama Didier Gomes akaridhika nao.

Biashara walikutana na Simba katika msimu huu mara mbili mchezo wa kwanza uliisha kwa sare ya bao 1-1, mabao yakifungwa na Inoccent Edwin na Clatous Chama ambaye hayupo katika kikosi cha mabingwa hao kwa sasa.

Mechi ya mzunguko wa pili Simba walipata ushindi wa mabao 2-0, katika Uwanja wa Karume ambao utatumika katika mchezo wa leo na mabao yote ya mabingwa hao watetezi yalifungwa na nahodha John Bocco.

Msimu wa pili ilikuwa 2019-20, Simba walishinda mechi zote mbili walianzia ugenini kwa mabao 2-0, ambayo yalifungwa na Meddie Kagere na Miraji Athumani ambaye msimu huu aliachwa na amejiunga na KMC.

Mechi ya mzunguko wa pili iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Simba walishinda mabao 3-1, ambayo yalifungwa na Kagere, Luis Miquissone na Francis Kahata ambao wawili hawa hawapo kikosini wakati bao wa Biashara lilifungwa na Novatus Dismas.

Msimu uliopita mechi ya kwanza Simba wakiwa nyumbani walishinda mabao 4-0, ambayo yalifungwa na Clatous Chama,Kagere na Chris Mugalu wakati mchezo wa marudiano mabingwa hao walishinda tena bao 1-0 wakiwa ugenini ambalo lilifungwa na Bernard Morrison. Tuko LIVE Musoma.