Mdamu: Ile ajali ni Mungu tu!

Monday September 13 2021
mdamu pic 1
By Yohana Challe

MUNGU Mkubwa! Ndivyo unavyoweza kusema ikiwa zaidi ya siku 60 za maumivu makali hatimaye, Gerald Mdamu sasa yupo nyumbani akicheza na familia yake.
Julai 9, 2021 itabaki kuwa kumbukumbu kwa wachezaji na uongozi wa timu ya Polisi Tanzania kutokana na ajali waliyoipata wakiwa wanatoka mazoezini Uwanja wa TPC wakijiandaa na michezo ya mwisho ya Ligi Kuu.
Katika ajali hiyo, Mdamu alivunjika miguu yote miwili na kuwahishwa Hospitali ya KCMC kwaajili ya matibabu na baadaye kuhamishiwa hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Mwanaspoti ambayo imekuwa ikiandika taarifa zake tangu tukio hili lilipotokea, imebahatika kupiga naye stori akiwa nyumbani kwake, ameeleza kilichotokea huku mkewe na nduguze nao wamefunguka.


MUNGU MKUBWA
Moja ya neno ambalo Mdamu amekuwa akilitamka kila wakati alipokuwa akipiga stori na Mwanaspoti ni Mungu Mkubwa, akiamini hadi hatua ya sasa aliyofikia ni mapenzi ya Muumba.
“Naona mabadiliko makubwa sana kwa siku hizi mbili tangu nimetoka hospitali kwani nyumbani napata kila kitu kwa muda ninaouhitaji lakini hospitali kuna changamoto zake.
“Ninachoshukuru zaidi daktari ameniambia nahitaji kama wiki tatu vidonda vitafunga na nitakaa sawa, kikubwa ameniambia nipunguze mawazo, nikubaliane na hali, hivyo nitaona mabadiliko na kila baada ya wiki mbili nitakuwa narudi hospitalini kwaajili ya uchunguzi zaidi.”


SAFARI YA SAUZI VIPI
Agosti 29, Benedicto Mdamu ambaye ni kaka wa Gerald aliiambia Mwanaspoti kuwa mdogo wake ataondoka kwenda Afrika Kusini katika Hospitali ya Vicent Palloti na kwa muda wote huo atakuwa chini ya daktari, Robert Nicholas huko Cape Town.

mdamu pic
Advertisement


Lakini siku moja kabla ya safari hiyo anasema mdogo wake aliingizwa chumba cha upasuaji jambo ambalo lilikwenda vyema na hatimaye Septemba 7 aliruhusiwa kurudi nyumbani lakini kwa uangalizi wa daktari kwa muda wote atakaokuwa nyumbani.
“Siwezi kueleza kitu gani kilitokea au madaktari waliona nini, lakini kikubwa kila kitu kinakwenda vyema kwa sasa na hata mwenyewe (Gerald) anasema anaona matumaini makubwa,” anasema Benedicto.
“Jambo jingine lililokwamisha safari kuna wadau wengi walijitokeza kutusaidia ikiwemo fedha, wengine tiketi za ndege hivyo taratibu zote zilikuwa sawa lakini ghafla siku moja kabla ya safari nikaona mabadiliko.
“Kila niliyekuwa nampigia simu kuhusu ahadi yake nikaona kama kuna kigugumizi yaani nikahisi kuna kitu nyuma ya hili maana hata uongeaji wao ulikuwa unanipa shaka hivyo sikuweza kujua nini kilitokea.”
Benedicto anasema ukosefu wa fedha ndio ilikuwa sababu kubwa ya safari yao kukwama sababu fedha nyingi hazikuwafikia mkononi licha ya ahadi zilizotolewa.
“Hata hivyo, daktari alituambia kwa sasa hali ya dogo (Gerald) iko vyema hivyo tuondoe wasiwasi maana tatizo lake hata Muhimbili linawezekana kutatuliwa hivyo tuwe watulivu.”


MKE WA MDAMU
Gerald ana mke anayeitwa, Juliana John na watoto wawili, Brayton Mdamu (6) pamoja na Yullia Mdamu mwenye mwaka mmoja kwa sasa.

mdamu pic 2


“Siku ya tukio nilikuwa Dar es Salaam, nikapata taarifa kuwa timu ya Polisi imepata ajali na Gerald amevunjika miguu yote, nilishtuka sana lakini nikawa kama sielewi.
“Ilipofika saa 10 jioni, Gerald alinipigia simu na kunisalimia yaani akaongea kama nilivyomzoea na hakuonyesha utofauti wowote, nikamuuliza wewe mzima? Akacheka kisha akajibu ‘Ndio mke wangu’.
“Nikamuuliza tena mbona nasikia umevunjika miguu yote miwili? Akajibu ‘sio kweli ila ni kweli tumepata ajali ila mimi niko sawa.”
Juliana anasema baada ya kuongea na mume wake akapata amani na kuendelea na shughuli zake lakini ilipofika jioni akawasha TV na kutazama habari na hapo akagundua mume wake amemdanganya.
“Nikachukua simu na kumpigia. Sikumpata hadi siku mbili zilipopita akanitafuta na kuniambia yeye mzima na siku inayofuata atakuja Dar es Salaam. Nikawa sielewi taarifa zinazoenea na maneno yake anayosema na hata kaka yake (Benedicto) naye alinificha akisema mdogo wake yupo sawa.
“Baada ya kuona siku tuliyokubaliana atarudi hakurudi, nikapanda gari bila kumwambia mtu yeyote. Nilipofika Moshi ndugu zake wakaniambia ukweli na kueleza mume wangu amebadilika.
“Gerald hataki kuongea na mtu, amekuwa mkali na anaongea kwa kufoka sana hivyo ukiingia ndani (wodini) kubaliana na matokeo utakayokutana nayo.”
“Nilipoingia ndani nikamkuta macho yake yamemtoka kwa hasira lakini ghafla aliponiona alicheka na nikamkumbatia akaniambia ‘nakupenda mke wangu’ na hali yake ikaanza kukaa sawa.”
Mdamu alizaliwa Desemba 7, 1997.


Advertisement