Mdamu anatia huruma, aomba msaada wa Watanzania

Thursday July 29 2021
mdamu pic
By Waandishi Wetu

STRAIKA wa Polisi Tanzania, Mathias Mdamu aliyevunjika miguu yote katika ajali iliyotokea hivi karibuni timu yake ikitokea mazoezini mjini Moshi anatia huruma. Amewaambia Watanzania kwa uchungu mkubwa huku akilia; “Naombeni mnisaidie, hali yangu mbaya.” Mdamu alihamishiwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam akitokea KCMC -Moshi.

Akizungumza na Mwanaspoti kupitia simu ya kaka yake, Benedicto Mdamu(pichani kabla ya ajali) alitamka maneno mazito yaliyoambatana na kilio kisha alishindwa kuendelea kuzungumza. “Nawaomba Watanzania kwa upendo wao, huruma zao, wanione na mimi kama wanavyowaona wengine ili nisaidiwe nitibiwe, lakini kama kilio changu kitamfikia na mama yangu Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anikumbuke mtoto wake ili nitibiwe kwa uharaka,” alisema huku akilia kwa uchungu na kaka yake akimtuliza na kumwambia amtumaini Mungu.

Awali Polisi wenyewe kupitia kwa Robert Munisi alidai kushangazwa na malalamiko yanayoibuka kila kukicha huku akisisitiza kwamba walihusika kumhamisha mchezaji huyo kutoka Moshi kwenda Dar na wanawasiliana na Mkewe kila mara kutoa msaada kwavile aliumia akiwa kazini. Mdamu ambaye ana watoto wawili Bryson (6) na Julian ambaye ni mchanga hajui hatima yao endapo kama atakosa matibabu ya haraka.

Straika huyo yupo na ndugu zake wa karibu ambao wanaweka wazi kuhitaji msaada wa hali na mali kutoka kwa familia ya soka nchini, ili atibiwe haraka kabla mambo hayajaenda kombo.

Benedicto anayemuuguza Mhimbili, ameeleza wanavyopitia wakati mgumu, huku mdogo wake akionekana kukata tamaa na kutoelewa hatima yake.

Aliliambia Mwanaspoti kwamba gharama zinazotakiwa kila siku anajikuta wakati mwingine anashindwa kuzimudu na kufanya mdogo wake awe mtu wa kulia kila wakati, huku akijiona hana thamani tena mbele ya uso wa dunia.

Advertisement

“Nitoe wito kwa wachezaji, makocha na wadau wa soka mbalimbali atakayeguswa na chochote amsaidie mdogo wangu ili aweze kutibiwa kwa haraka kabla ya mambo kuendelea kuwa mabaya, maana muda unavyokwenda ndivyo anavyojisikia vibaya,” alisema.

“Bora niwe muwazi ili asaidiwe, najua kuna wachezaji ambao wataguswa na kama wanataka kuamini wanaweza wakaja kujionea wenyewe, sijui hata niseme nini hata kama kuna kiongozi atasikia kilio changu naomba atusaidie na Mungu atambariki.”


MKE ATOA NENO

Mkewe Mdamu aliyejitambulisha kwa jina la Julian Marekela licha ya kuongea kwa hofu na huzuni kubwa alizungumza machache na kuwaomba Watanzania wamsaidie mumewe apone.“Naomba msaada ili mume wangu atibiwe kwa haraka maana ana hali mbaya, sijui hata nifanye nini,” kisha akakata simu na kuendelea kulia kwa uchungu.


BARAZA AMSIKITIKIA

Kocha Francis Baraz ambaye aliwahi kumfundisha Mdamu timu ya Biashara United kabla hajahamia Polisi Tanzania, alisikitishwa na hali yake.

“Nimemfundisha nikiwa Biashara United, zilinishtusha sana taarifa zake, Mdamu alikuwa na ndoto kubwa sana katika soka, naamini ipo siku zitatimia,” alisema.


Kwa yeyote ambaye atapenda kumsaidia Mdamu awasiliane kwa simu ya kaka yake namba 0714 - 716843.

Advertisement