Mbongo atwaa ubingwa Qatar

NYOTA mwenye asili ya Tanzania, Akram Afif ametwaa ubingwa wa Kombe la Qatar baada ya chama lake, Al-Sadd SC linalonolewa na fundi wa zamani wa Barcelona, Xavier Hernandez ‘Xavi’ kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Al Duhail.

Mabao ya mawili ya mshambuliaji wa Kimataifa wa Algeria, Baghdad Bounedjah yalitosha kwa kwa Al-Sadd SC kutawazwa kuwa mabingwa wa kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo wakiwa kwenye uwanja wa Abdullah bin Nasser bin Khalifa huko Doha.

Akram ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Simba, hakuwa sehemu ya kikosi cha chama la Xavi kilichocheza mchezo huo kutokana na kukabiliwa kwake na adhabu ya kukosa michezo miwili kutokana na kauli aliyoitoa baada ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Al Rayyan.

Mchezaji huyo mwenye asili ya visiwani Zanzibar, alisema,”Tumecheza dhidi ya wachezaji 11 uwanjani huku akiwepo mwingine wa ziada upande wao.” Kauli hiyo ilitafsiriwa kwamba winga huyo , alikuwa akimshambulia wazi mwamuzi wa mchezo huo.

Akram ambaye anamabao matano na asisti nane kwenye michezo 10 ya Ligi Kuu nchini humo, alikuwa kwenye kiwango bora kwenye mchezo huo wa nusu fainali ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lakini alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi huyo.

Kwa mujibu wa kanuni, mchezaji huyo mwenye asili ya Tanzania, imebidi afungiwe huku akitakiwa kulipa faini ya QR 30,000 (Sh. 19 milioni).

Licha ya kukosekana kwa Akram, chama la Xavi halikuyumba kwenye mchezo huo wa fainali maana alikuwepo fundi mwingine ambaye aliwahi kutamba akiwa na washika mitutu wa London, huyo si mwingine ni Santi Cazorla.

Ubingwa huo ulikuwa ni wa tano kwa Xavi tangu apewe kibarua cha kuinoa miamba hiyo ya soka la Qatar, “Ninafuraha na kiwango ambacho timu imekionyesha. Tulikuwa kwenye kiwango bora na matokeo yameakisi ubora wa kiwango chetu, tulicheza kwa nguvu na kujitoa.”

“Haikuwa kazi nyepesi kuwadhibiti wapinzani wetu kwa sababu haikuwa timu dhaifu. Walitupa wakati mgumu kipindi cha pili, huwa kawaida kwa michezo ya fainali huwezi kumiliki mpira kwa vipindi vyote viwili kuna muda lazima uangaike ndivyo ilivyokiuwa,” alisema.

Xavi aliongeza kwa kusema,”Kwa ubingwa ambao tumetwaa umethibitisha kuwa sisi ni bora Qatar.”