Mayay: Dabi hii anapigwa mtu

Muktasari:

MASHABIKI wa Simba na Yanga wanahesabu masaa tu, ili kulishuhudia pambano la watani wa jadi, linalotarajiwa kupigwa kesho Jumamosi ya Mei 7, 2021 Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.

MASHABIKI wa Simba na Yanga wanahesabu masaa tu, ili kulishuhudia pambano la watani wa jadi, linalotarajiwa kupigwa kesho Jumamosi ya Mei 7, 2021 Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam.

Mechi hiyo itapigwa saa 11:00 jioni, ambapo dakika 90 ndizo zitakazomaliza ubishi wa nani atalala mapema, kutokana na tambo zinazoendelea kwasasa kutoka kwa mashabiki hao.

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay amesema ana uzoefu na dabi hiyo, amesimulia namna zamani walivyokuwa wanaandaliwa kuelekea mchezo huo na asili ya ushindani ulivyo baina ya klabu hizo.

"Zamani kama wachezaji tulikuwa tunadai, viongozi walikuwa wanatulipa kabla ya mechi,tulihamasishwa hilo lilifanya hata kama timu ipo chini ya kiwango, ikiingia uwanjani inakuwa na ushindani mkubwa ambao hauwezi kutabiri nani anaweza akashinda mechi,"amesema na ameongeza kuwa;

"Kwa jicho la ufundi Simba ipo vizuri kila idala, inacheza kwa kombinesheni, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja unaonekana, kocha anaijua timu yake kujua ni jinsi gani ya kubadili matokeo kwa muda wowote, Yanga naiona changamoto kwa Nabi bado hajazoeana na wachezaji wake na bado hana kikosi cha kwanza,"amesema.

Amesema mchezo wa kesho licha ya kwamba Yanga haipo vizuri, anaona utakuwa mchezo mgumu na waushindani endapo kama Wanajangwani wataingia mbinu ya kushambulia kwa kushitukiza na sio kuchezea mpira kama Simba.