Matola: Bado sita tu, Polisi wakubali yaishe

Muktasari:

Katika mchezo huo kila timu ilipambana haswa kipindi cha pili, lakini Simba iliweza kuondoka na pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 kupitia kwa nyota wake wa kimataifa, Luis Miquissone.

Mwanza. Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini amesema makosa waliyoyafanya nyota wake haswa kucheza faulo nyingi ndizo ziliwapa wapinzani nafasi ya kuondoka na alama tatu.

Pia ameongeza kuwa kimbinu wamefanikiwa lakini ishu ya uzoefu kwa vijana wake dhidi ya nyota wa Simba imechangia katika hali fulani kujikuta wakipoteza mchezo huo muhimu.

"Niliwataarifu mapema wachezaji wangu waepuke sana mipira ya faulo lakini mchezaji wangu alimkwatua mpinzani na kusababisha wanapata bao la moja kwa moja, lakini kimbinu tulifanikiwa tatizo ni uzoefu" amesema Hamsini.

Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman amesema waliingia uwanjani wakifahamu mechi kuwa ngumu na kwamba wanashukuru kwa kuweza kuondoka na pointi tatu ambazo zinawaweka katika mbio za Ubingwa.

Ameeleza kuwa baada ya mechi ya leo wanahitaji pointi sita tu ili kutangaza Ubingwa na kwamba ishu ya kupata bao moja tofauti na mechi zilizopita ni kawaida kwani siku hazilingani na straika wao hawakutumia vyema nafasi walizopata.

"Tunahitaji pointi sita tu baada ya leo, tumepata nafasi nyingi lakini Straika wetu hawakuzitumia vyema ila yote yote tunashukuru kwa pointi tatu ambazo zinatubakiza juu kwenye msimamo" amesema Matola.