Mastaa wote Simba kambini, kuwasoma Wabotswana

Kocha msaidizi wa Simba, Hitimana Thierry alisema hawana muda wa mapumziko kwa wachezaji kwani wana siku 10 tu za maandalizi kabla ya mchezo na Jwaneng Galaxy FC.

Alisema baada ya kuliona hilo wachezaji ambao wapo timu za taifa wanaamini watakuwa wanafanya mazoezi ya nguvu na watacheza mechi mbili, pamoja na hilo watakuwa wakiwafuatilia.

“Hawa waliobaki katika timu tutaanza nao mazoezi mepesi, kisha baada ya hapo tutakwenda kwenye mbinu ambayo na wale waliokuwa timu za taifa wataungana na wenzao katika hili,” alisema.

“Baada ya hapo tutakuwa na muda mwingi wa awamu ya kuangalia mechi za Galaxy - zile za mashindano ya kwao na mchezo wa hatua ya kwanza waliocheza kisha kufahamu ubora na upungufu waliokuwa nayo.”

“Tukipata taarifa nyingi za kiufundi kutokana na kuwafuatilia tutahamishia uwanjani kwa wachezaji ili kufahamu wanakwenda kushambulia vipi kutokana na upungufu wa wapinzani na tunazuia namna gani kutokana na ubora wao.

Kutokana na mipango tuliyonayo kwa wachezaji na mbinu ambazo tutazifanya wakati huu, nina imani kubwa tutakwenda kufanya vizuri katika michezo yote miwili dhidi ya Galaxy na kufuzu hatua ya makundi.”

Katika hatua nyingine, Hitimana alisema kikosi chao kitaondoka wiki ijayo kwenda Botswana kikiwa na nyota wote 31 waliowasajili kwenye mashindano hayo.

“Kadri siku zinavyozidi kwenda maandalizi tunayofanya kikosi chetu kinaendelea kuwa na muunganiko kwa wachezaji wapya na wale waliokuwepo msimu uliopita naamini tutakuwa bora zaidi,” alisema.

Wachezaji wa Simba walioitwa Taifa Stars ni Aishi Manula, Mohammed Hussein, Kennedy Juma, Israel Mwenda, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na John Bocco.