Mastaa wapya wazalisha mabao 15

MKIKI Mikiki ya Ligi Kuu Bara inaendelea huku timu shiriki zikiwatumia wachezaji wake wapya ziliowasajili kwenye Dilisha Dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu na baadhi ya timu kuonekana kuanza kunufaika na mastaa wapya ziliowasajili.
Hadi mastaa wapya walioingia dirisha dogo kwenye timu tofauti wamezalisha jumla ya mabao 15, ambapo 10 yamefungwa moja kwa moja na mastaa hao huku tano zikiwa ni asisti kutoka kwao.
Nyota mpya wa Simba Mrundi, Said Ntibanzokiza 'Saido' aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja na nusu akitokea Geita Gold ndiye anaonekana kulipa zaidi kati ya wengi waliosajiliwa dirisha dogo baada ya kuhusika katika mabao sita ya Wekundu wa Msimbazi hao, akifunga matano na kutoa asisti moja kwenye mechi tatu za ligi alizocheza.
Katika mechi yake ya kwanza ndani ya Simba, staa huyo wa zamani wa Yanga alianza kwa kupiga mabao matatu 'hat trick' na asisti moja ambapo chama lake hilo jipya liliichakaza Tanzania Prisons kwa mabao 7-1 na baada ya hapo alifunga mabao mawili kwenye mechi iliyofuata dhidi ya Mbeya City, Simba ikishinda 3-2.
Polisi Tanzania pia imeonekana kuvuna zaidi mabao kutoka kwa wachezaji waliosajiliwa kwenye dirisha dogo kwani katika sare ya 3-3 iliyoipata mbele ya Coastal Union, mabao yake mawili yalifungwa na Kelvin Sabato 'Kiduku' ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu atue kikosini hapo akitokea Singida Big Stars, lakini pia katika mchezo uliofuata nyota wake Mpya Mkongomani, Enock Mayalla aliipa ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Namungo na mabao yote akiyafunga yeye na huo ukiwa mchezo wake wa kwanza kwa maafande hao.
Staa wa zamani wa Mtibwa Sugar aliyetua Mbeya City akitokea Dodoma Jiji Salum Kihimbwa, naye ameanza kwa kasi akitoa asisti ya kwanza kwa kwenye moja ya bao dhidi ya Simba licha ya timu yake kuchapwa 3-2 ukiwa ni mchezo wa kwanza kwake ndani ya Wabishi hao wa Mbeya lakini pia mchezo uliofuata dhidi ya Mtibwa Sugar alitoa pasi ya bao kwa Sixstus Sabilo akifunga bao pekee na la ushindi kwenye mechi hiyo.
Nyota wa zamani wa Simba Elias Maguri, naye alianza maisha mapya ndani ya Geita Gold kwa kutoa asisti ya bao la pili na la ushindi chama lake likiilaza 2-0 Dodoma Jiji, lakini pia mechi iliyofuata alitoa asisti kwa Seleman Ibrahim katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania.
Staa mpya wa Simba, Mkongomani Jean Baleke, naye alianza vyema maisha yake ya soka Tanzania baada ya kupachika bao pekee na la ushindi katika mechi yake ya kwanza ndani ya Wanamsimbazi hao dhidi ya Dodoma Jiji juzi Jumapili mechi ikiisha 1-0.
Sambamba na hao, Singida Big Stars nayo imenufaika na usajili mpya wa straika Mkongomani, Fancy Kazadi, kwani aliiwezesha kufika fainali ya Kombe la Mapinduzi akifunga jumla ya mabao sita na kuibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.
Kazadi alianza vyema ndani ya Singida akifunga bao moja kwenye mechi ya kwanza ya Mapinduzi Cup dhidi ya KMKM, akafunga tena moja mbele ya Yanga na kutupia manne, dhidi ya Azam na kutinga fainali lakini chama lake likalala 2-1 mbele ya Mlandege.
Mastaa wa Simba, Saido na Baleke kila mmoja kwa wakati wake aliliambia gazeti hili kufurahishwa na mwanzo mzuri kwa kufunga bao kwenye mechi zao za kwanza na kuahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi huku winga mpya wa Mbeya City, Kihimbwa naye akifurahishwa na ubora wake.
"Nashukuru kwa kuanza vyema ndani ya Simba, naamini kadri siku zinavyosonga nitazidi kuimarika na kuzoeana na wenzangu na kufikia malengo ya timu," alisema Saido.
"Tunapambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri hivyo nafurahi ninapochangia hilo kwani ni jukumu langu kufanya hivyo," alisema Kihimbwa.