Mashindano ya Top Model yarejea, mshindi kulamba Sh5 milioni

Muktasari:

Hatimaye mashindano ya kumsaka Mwanamitindo Bora 'Top Model' yamerejea ambapo sasa yatafanyika Februari mwakani.

Hatimaye mashindano ya kumsaka Mwanamitindo Bora 'Top Model' yamerejea ambapo sasa yatafanyika Februari mwakani.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Oktoba 16, 2021 na Mkurugenzi wa Kampuni ya mavazi ya 'Paka Wear', Gymkhana Majaliwa ambao ndio waandaji wa mashindano hayo kwa sasa wakiwa wameyachukua kutoka kwa Jackson Kalimtima ambaye ndiye muasisi wake.

Majaliwa amesema mashindano hayo yaliyofanyika mara ya mwisho mwaka 2014 yamerudi kwa nia ya kukuza na kudumisha tasnia ya mitindo hapa nchini ambayo ina fursa nyingi za ajira kwa mtoto wa kike.

"Ni mashindano ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2014, lakini yalifungua fursa nyingi za ajira na kwa kutambua umuhimu wake tumeona tuyaendeleze," amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Mratibu wa programu hiyo kutoka Paka Wear, Adili Kigoda amesena katika mashindano hayo mshindi wa kwanza atapata Sh5 milioni, wa pili Sh2 milioni na wa tatu Sh1 milioni huku watakoishika nafasi  ya nne mpaka ya kumi watapata cheti cha ushiriki na nafasi ya kufanya kazi na kampuni yao.

Wakati kuhusu sifa za mtu atakayependa kushiriki mashindano hayo, Kigoda amesema awe Mtanzania, awe na miaka 18 hadi 25, mrefu kuanzia futi 5.7, ajue kuongea kwa ufasaha lugha ya kiswahili na kingereza na awe mzalendo na mwenye maadili.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Seleman Khalifa amesema Baraza limebariki mashindano hayo na wapo tayari kutoa ushirikiano muda wowote watakapohitajika.

Khalifa ambaye ni ofisa Sanaa wa Basata,aliwasihi wasichana wenye sifa kujitokeza kwa wingi kwa kuwa mbali ya kupata fursa ya ajira pia watakuwa wanaikuza tasnia ya uanamitindo.

Mary Chizi ambaye ni mkufunzi wa wanamitindo watakaoshiriki mashindano hayo, amesema wamejipanga kuwapika wasichana watakaoshiriki ambao wataweza kuitangaza nchi vizuri ndani na nje ya nchi.