Mashabiki waungana kisa kuahirishwa Kariakoo Dabi

Muktasari:

MASHABIKI wa Simba na Yanga wamechefukwa na wameamua kuungana kwa pamoja kupinga kilichochotea jana Jumamosi, kuahirishwa mechi ya Dabi.

MASHABIKI wa Simba na Yanga wamechefukwa na wameamua kuungana kwa pamoja kupinga kilichochotea jana Jumamosi, kuahirishwa mechi ya Dabi.

Simba na Yanga zilikuwa zicheze saa 11:00 jioni lakini badae ukasogezwa muda hadi 1:00 usiku, hivyo sintofahamu hiyo mchezo ukaahirishwa na kuacha maswali mengi kwa wadau wa soka nchini.

Mwanaspoti limepata mtaani Dar es Salaam kuzungumza na mashabiki wa klabu hizo kujua walivyopokea tukio hilo, limewakuta na hasira wakilitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Michezo wawape majibu yaliyoshiba ili kurejesha Imani ya kuzingatia kanuni za soka.

Shukuru Carlos ni shabiki wa Yanga lialia ameliambia Mwanaspoti online kwamba kilichotokea jana kimeondoa hamasa ya kwenda uwanjani.

"Kama wanataka tuwe na morali ya kushabikia timu zetu uwanjani Wizara ya michezo na TFF waje na majibu yaliyoshiba na watuombe msamaha kwa maumivu waliotupa,"amesema.

Hoja yake imeungwa mkono na shabiki wa Simba, aliyejitambulisha kwa jina la Tariq Seif amesema katika hilo halijawachefua Yanga pekee, Bali limewanyongonyeza na kuonekana hawana thamani.

"Kuna watu kwenye Tawi letu hili la Simba mpira pesa na Maendeleo lililopo Faya, Kariakoo tumewapokea kutoka mikoani na nje ya nchi, je hao watakuja tena, tumekosewa sana, tunahitaji majibu sahihi,"amesema.

Naye Yusuph Mkaliamboga shabiki wa Yanga ambaye amekutwa kwenye kijiwe cha Faya Kariakoo, Dar eS salaam, ameungana na wenzake kwamba timu hizo zina tamaduni zake na sio ya kukurupuka na maamuzi.

"Simba walijua watachapwa mabao 2-0 hiyo saa 1:00 usiku Kiarabu ni siku nyingine kwa hiyo matokeo yangegeuka, lakini pia zinatumia gharama kubwa katika maandalizi yao,"amesema na ameongeza kuwa;

"Kikubwa vyombo husika bike na majibu kamili kuondoa dharau hii walioifanya lasivyo wakimaliza kimyakimya wataweka mpasuko mkubwa sana,"amesema.