Mashabiki nyomi nje kwa Mkapa

MAELFU ya mashabiki wa Simba wametapakaa nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa wakifuta utaratibu wa kuingia ndani kushuhudia mastaa wao wapya kuelekea msimu mpya

Simba leo inaadhimisha tamasha la Simba Day likiwa ni la 14 tangu lilipoanzishwa "Sisi tunaujaza leo hatuna jambo dogo," ni kauli za mashabiki waliojitokeza kwa wingi.

Ulinzi mkubwa uliowekwa na unawafanya mashabiki wa timu hiyo kuingia taratibu bila ugomvi wakiwa chini ya usalama.

Wakati huo huo watani zao Yanga wamejitokeza kushuhudia watani zao wakiadhimisha kilele cha tamasha la Simba Day.


KAGERE, MUGALU WAKUMBUKWA
Pamoja na uongozi wa Simba kuwaaga wachezaji wao, Meddie Kagere, Chris Mugalu washambuliaji na kiungo Thadeo Lwanga nyota hao wametawala kwenye mabango kwa Mkapa.

Kagere, Mugalu na Lwanga wameachwa na Simba kutokana na kushindwa kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo.

Kagere ambaye amejiunga na Singida Big Stars amejitokeza kwenye mabango ya mashabiki wa Simba waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tamasha la Simba Day.

Mbali na Kagere pia mashabiki walibeba mabango yaliyoandikwa majina ya Lwanga na Mugalu wakiwatakia kila la kheri kwenye maisha yao mpya ya soka pamoja na kuwashukuru kwa kile walichokifanya wakiwa Simba.