Manula amtetea Kibu

MAMBO yamezidi kuwa magumu kwa mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis baada ya kushindwa kuonyesha ubora tangu msimu uanze jambo lililozua hisia tofauti kwa mashabiki, lakini kipa wa timu hiyo, Aishi Manula amemtetea straika wao kuwa ana uwezo mkubwa.

Kibu ndiye mfungaji bora wa Simba msimu uliopita aliomaliza na mabao manane, lakini hadi sasa timu yake ikiwa imecheza mechi 11 hajafunga bao na kiwango chake kinaonekana kuporomoka jambo linalomuumiza yeye mwenyewe na wapenzi wa timu hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Manula ambaye ni nahodha msaidizi namba tatu wa Simba, aliwataka mashabiki kuacha kumzomea Kibu na wampe moyo kwani ana nafasi ya kufanya vizuri.

“Ni kipindi cha mpito kwake. Tunahitaji kumpa moyo zaidi ya kumzomea, hiyo ni njia nzuri itakayomrudisha kwenye ubora kwani ni miongoni mwa wachezaji bora tulionao kikosini na tuko pamoja kwenye kila jambo,” alisema Manula.

Naye kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda alimtetea Kibu akisema ni mchezaji mzuri na mpambanaji ambaye licha ya makosa anayofanya uwanjani, lakini ana mazuri yake.

“Watu hawapaswi kumbeza Kibu. Ni mchezaji mzuri na yupo Simba kwa ajili ya kucheza. Kinachotokea kwake humtokea yeyote kwenye jambo analofanya hivyo sio sahihi kumbeza na kumzomea,” alisema.

“Ana mazuri yake. Kwa hiyo mimi kama kocha nimeyachukua na nitayafanyia kazi na mwisho wa siku atakuwa sawa na kuendelea kuipambania timu.”

Staa huyo aliyejiunga Simba msimu uliopita akitokea Mbeya City, amefunguka kutofurahishwa na kinachomtokea kwa sasa lakini anaamini ni jambo la mpito na muda si mrefu atarejea kwenye makali yake.

“Hakuna mchezaji anayependa kufanya vibaya. Ni kipindi cha mpito tu ambacho kinamtokea kila mtu, lakini naamini nitaimarika na kuwa bora zaidi ndani ya muda mchache ujao,” alisema Kibu.

Pamoja na kuonekana kutofanya vizuri, Kibu ni miongoni mwa washambuliaji waliocheza dakika nyingi ndani ya chama hilo hadi sasa msimu huu, pia ana asisti moja aliyompa pasi ya kichwa Jonas Mkude na kufunga bao pekee na la ushindi dhidi ya Prisons.