Prime
Manula afunguka hatma yake Simba
Muktasari:
- Hata hivyo, tangu msimu uliopita, Manula amekuwa na ingia toka katika kikosi cha kwanza ambapo amecheza mechi chachem huku makipa wa kigeni Ayoub Lakred na Moussa Camara wakiamini na hivyo kumuweka benchi.
KIPA wa Simba, Aishi Manula kwa sasa hana namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo licha ya kuipa mafanikio kibao ikiwamo ubingwa wa Ligi Kuu Bara zaidi ya mara nne tangu alipotua kikosini 2017/18.
Hata hivyo, tangu msimu uliopita, Manula amekuwa na ingia toka katika kikosi cha kwanza ambapo amecheza mechi chachem huku makipa wa kigeni Ayoub Lakred na Moussa Camara wakiamini na hivyo kumuweka benchi.
Cha ajabu, kipa huyo ameonekana kana kwamba ni chagua la tano kwani mbali ya wageni hao wawili, lakini Ally Salim na Hussein Abel wamewahi kupata nafasi ya kucheza ilhali yeye hachezi na katikati ya yote Manula amefunguka mambo kadhaa.
Manula amesema licha ya kutopata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza mara kwa mara, atahakikisha anafanya majukumu yake ipasavyo, huku akiweka wazi klabu hiyo bado ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo amezungumza hayo wakati akiwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyokuwa ikicheza mechi za kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) itakayofanyika Februari 2025 katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Manula ambaye tangu kuanza kwa msimu huu hajacheza mechi yoyote ya kimashindano ndani ya Simba, amesema: "Ni kweli usipopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kuna muda unapoteza hali ya kujiamini lakini niseme wazi nitapambana mazoezini kwa ajili ya timu kiujumla, ushindani ni mkubwa lakini nitaendelea kuonyesha uwezo wangu kadri iwezekanavyo."
Kipa huyo ambaye mara ya mwisho kuichezea Simba ilikuwa ni katika mechi ya kirafiki dhidi ya Al Hilal ya Sudan iliyopigwa Agosti 31, mwaka huu na kuisha kwa sare ya bao 1-1, anaamini nafasi yake kikosini hapo ipo na muda ukifika atacheza.
"Kuhusu ubingwa naamini Simba ina nafasi kubwa ya kuchukua na hayo ndiyo malengo yetu, natambua mashabiki wanataka pia kuniona nikicheza kama leo (juzi) nikiwa na Stars, nawaahidi nitapambana kwa kufanya mazoezi na jukumu la kucheza lipo kwa benchi la ufundi, naamini ipo siku nitacheza," alisema.
Manula alionyesha uwezo mkubwa hadi kupachikwa jina la 'Tanzania One', jambo ambalo halikuja kwa bahati mbaya kwani tangu ajiunge na Simba ametwaa mataji yote ya ndani yakiwemo ya Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Pia amebeba Kombe la FA msimu wa 2019/20 na 2020/21 na Ngao ya Jamii mwaka 2017, 2018, 2019, 2020 na 2023.
Mbali na mataji hayo, pia amechukua tuzo binafsi huku akikiwezesha kikosi hicho kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne katika misimu sita huku mara nyingine moja ya tano ikiwa ni ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Kipa huyo aliyejiunga na Simba msimu wa 2017/2018 akitokea Azam FC, amekosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa, Ayoub Lakred kutokea FAR Rabat ya kwao Morocco na sasa alipotua Moussa Camara kutoka Horoya AC ya Guinea.
Baada ya kuumia kwa Ayoub wakati kikosi hicho kikiwa katika maandalizi ya msimu (Pre Season), wadau wengi walitegemea kumuona Manula akidaka lakini imekuwa ni tofauti, kwani Camara ameingia moja kwa moja kwenye mfumo wa kocha, Fadlu Davids.
Kuonyesha imani kubwa ya Fadlu ipo kwa Camara eneo la kipa, katika michezo tisa ya Ligi Kuu Bara ambayo Simba imecheza msimu huu, amedaka yote na kati ya hiyo ni miwili tu ambayo ameruhusu bao, hivyo amekuwa na 'clean sheets' saba.
Kabla ya kujiunga na Simba msimu huu, Camara alichukua tuzo ya kipa bora mara mbili katika Ligi Kuu ya Guinea akiwa na kikosi hicho cha Horoya, huku akikiwezesha kutwaa mataji manne ya Ligi, FA akichukua mara tatu na Super Cup mara mbili.
Ukimuweka kando, Manula, Camara na Ayoub, makipa wengine ndani ya kikosi cha Simba ni Ally Salim ambaye kwa sasa ndiye kipa namba mbili baada ya Camara, mwingine ni Hussein Abel.