Mangungu: Nguvu moja iwe ya kumaanisha

MGOMBEA wa nafasi ya uenyekiti Simba, Murtaza Magungu ameendelea na kampeni zake za kuomba kupigiwa kura na wanachama wa timu hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili, Januari 29.
Leo amefanya kampeni hizo Manzese, Dar es Salaam ambapo amesisitiza kauli mbio ya Simba nguvu moja iwafanye wawe na umoja wa kuleta maendeleo ya klabu na usiwe msemo usiyotenda kazi.

Mangungu ambaye anamaliza muda wake wa uenyekiti na kugombea tena ndani ya klabu hiyo, amesema wanahitaji kuiona Simba inafanya vizuri kuanzia Ligi ya ndani hadi ya Mabingwa Afrika.
"Tayari Simba imeonyesha mwanga wa kufanya vizuri CAF tunahitaji kufanya muendelezo huo, kwani naamini timu inapofanya vizuri ndio furaha ya mashabiki na wanachama," baada ya kusema hivyo, zikasikika kelele kutoka kwa baadhi yao wakishangilia hoyooo.

Wakati anaendelea kutoa ushawishi wa kuchaguliwa, ilisikika Adhana ikamlazimu kukatisha akapata muda wa kuswali na kuwaruhusu wengine kufanya hivyo.

Baada ya kumaliza aliendelea na kunadi sera zake, namna anavyotaka kutoa mchango wake wa kuifanya Simba iwe tishio ndani na kimataifa.

"Tunaposema Simba nguvu moja basi asiwepo mwingine ambaye atakuwa anakwenda kinyume na kauli hiyo. Pia tukitaka kuongeza mapato kwenye timu, matawi kama wana kitu cha ubunifu watatakiwa kukipeleka kwenye mtandao wetu ambao unatuingizia pesa,"


HALI HALISI ILIVYOKUWA
Wakati wanaogombea ujumbe na Magungu mwenyewe anaongea wapo wanachama ambao waliendelea na stori zao, huku wengine wakiwa sehemu wanakouza vinywaji waliendelea na starehe zao.

Lakini wapo ambao walikuwa na uvumilivu wa kuendelea kukaa kwenye viti wakiwasikiliza wagombea sela zao.