Manara na Senzo watambiana

MSEMAJI wa klabu ya Simba Haji  Manara na Mshauri wa Uongozi wa Yanga, Senzo Mazingisa wameonesha kutambiana kwenye ukurasa wa Instagram ambapo kila mmoja amejinasibu kuwa bora zaidi.

Kupitia mtandao wa Instagram kwenye kurasa rasmi ya Haji Manara amechapisha picha ya Senzo akiwa amevalia jezi ya timu ya taifa ya Nigeria na kuandika:

" Upo wapi? ni muda mrefu tango nimekuona ama kukusikia, haujambo? naamini popote ulipo upo salama, kama litatokea lolote kwako tafadhari usinifiche, nina mfumo naweza kukupeleka Ihefu ukawa mkurugenzi mtendaji wao," aliandika  Manara.

Baada ya muda mchache kupita tangu Manara achapishe ujumbe huo,naye Senzo alikuja kwenye ukurasa ule ule wa Manara na kujibu hivi:

"Rafiki yangu nipo salama, nashukuru kwa kunicheki lakini unanamba yangu, ungenitafuta huko. Au ulikuwa unasubiri ruhusa kutoka kwa Trump ili unitafute? naelewa hautaki matatizo. Heri ya mwaka mpya, nipo kazini ndugu yangu nilikua na rikizo fupi ya kwenda kuiona familia yangu hivyo usijali kuhusu mimi, tupo kwenye mambo ya msingi zaidi ikiwemo mabadiliko ya kimfumo ya klabu yetu ya Yanga pia tunakaribia kuzindua mbio ziitwazo Mwananchi Marathon mapema mwaka huu, kwa bahati mbaya nilisahau kuwa hauelewi hiyo mipango na kila kitu kinachoendelea kwenye taasisi,".

Kupitia tambo hizo mashabiki kama kawaida wamegawana upande wa kusapoti kile wanayemkubali amekisema.

Ikumbukwe Senzo alijiunga na Yanga mwezi Agosti mwaka jana akitokea Simba.