Manara amponza Hersi

Manara amponza Hersi

SEKRETARIETI ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungulia mashtaka ya kimaadili Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na aliyekuwa ofisa wa klabu hiyo Haji Manara.

Taarifa iliyotolewa na TFF ilieleza licha ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo hivi karibuni kumfungia miaka miwili Manara kutojihusisha na shughuli yoyote za Mpira wa Miguu (any football related activity) ila
ameshindwa kutekeleza adhabu hiyo.

Kwa upande wa Injinia, Said amefunguliwa mashtaka kwa kwenda kinyume na ibara ya 16(1)(a) ya katiba ya TFF pamoja na ibara ya 1(6) ya katiba ya Yanga.

Baada ya Manara kuadhibiwa na Kamati hiyo, Sekretarieti ilimwandikia barua Injinia Hersi kuhakikisha klabu yake inaheshimu uamuzi huo.

Barua hiyo ilieleza, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF tayari amepelekewa mashtaka hayo na walalamikiwa watapewa mashtaka na mwito mara baada kamati hiyo kupanga tarehe ya kusikiliza mashtaka hayo.

Hatua hii inajiri baada ya Manara kuonekana kwenye kilele cha 'Wiki ya Wananchi' akitambulisha wachezaji na benchi la ufundi licha ya yeye mwenyewe kudai alikuwa ni mshereheshaji wa mtaani na hajajihusisha na soka.

Hivi karibuni Manara alifungiwa kutojihusisha na masuala ya michezo ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka miwili na faini ya sh20 milioni kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa Rais wa (TFF) Wallace Karia wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Coastal Union uliopigwa Julai 2 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.