Mambo manne yamemkwamisha Samatta England

MAMBO manne yanayonekana kuchangia kukatisha mkataba wa miaka minne wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Mfumo na mbinu za benchi la ufundi, mabadiliko ya mkurugenzi wa ufundi, usajili wa nyota wapya lakini pia takwimu zisizoridhisha tangu aliposajiliwa - kwa namna moja au nyingine kuifanya Aston Villa iamue kumuuza Samatta kwenda Fenerbahce ya Uturuki, uhamisho uliokamilika rasmi juzi, Ijumaa.

Fenerbahce, imemsajili kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, wenye kipengele cha kumsajili jumla kwa miaka minne ukiwa na kipengele kuwa klabu hiyo ya Uturuki imelazimika kulipa kitita cha Euro 6.5 milioni (Sh 17.6 bilioni) kwa Villa ili ipate huduma ya mshambuliaji huyo. Uhamisho huo wa Samatta umefanyika huku akiwa ameitumikia timu hiyo kwa muda wa takriban miezi nane tangu alipojiunga nayo mwezi Januari mwaka huu kwa dau la Euro 9.5 milioni (Sh 25.6 bilioni) akitokea KRC Genk ya Ubelgiji.

Takwimu zimemuangusha Samatta

Mabao 76 na pasi za mwisho 20 alizopiga katika jumla ya mechi 191 alizoicheza KRC Genk, hapana shaka ni takwimu zilizoishawishi Aston Villa kutumia kitita cha Euro 9.5 milioni (Sh 25.6 bilioni) kumnasa mshambuliaji huyo wa zamani wa TP Mazembe na Simba ikiamini kuwa itatibu tatizo la ubutu katika safu yake ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inayumba.

Hata hivyo kilichokuja kutokea kilikuwa ni tofauti hapo baadaye kwani licha ya Samatta kuanza vyema kwa kufunga bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Bournemouth na pia akipachika lingine katika mechi ya fainali ya Kombe la Calabao, Samatta alijikuta katika wakati mgumu katika idadi kubwa ya mechi zilizofuata ambazo hakuweza kupachika bao wala kupiga pasi ya mwisho.

Alicheza kwa dakika 90 tu katika mechi tano za Ligi Kuu ya England na katika idadi kubwa ya mechi alicheza kwa muda mfupi tofauti na matarajio ya wengi.

Katika kipindi hicho cha miezi minane aliyoichezea, Samatta alicheza mechi 16 za mashindano tofauti akifunga mabao mawili bila kuwa na pasi ya mwisho, lakini hata pia kupiga mashuti yaliyolenga bao yasiyozidi matano.

Usajili wa nyota wapya

Ni kama takwimu tajwa hapo juu ziliipa wasiwasi Aston Villa ambayo iliamua kufanya usajili wa washambuliaji wapya wawili - Ollie Watkins kutoka Brentford kwa dau la Pauni 28 milioni (Sh82 bilioni) na pia Bertrand Traore kutoka Olympique Lyon kwa dau la Pauni 17 milioni (Sh 50 bilioni). Bahati mbaya kwa Samatta, ndani ya muda mfupi, Watkins amepachika mabao mawili katika mechi mbili tofauti za Kombe la Calabao dhidi ya Burton Albion na Bristol City. Mchezo huo dhidi ya Bristol City ambao Samatta hakucheza, Traore ambaye alikuwa anaichezea Villa kwa mara ya kwanza naye aliifungia bao moja jambo ambalo ni wazi liliondoa uwezekano wa Samatta kuendelea kupata nafasi ya kucheza na hapana shaka kikaifanya timu hiyo kupata nguvu ya kuchukua maamuzi ya kumuuza.

Mabadiliko ya Mkurugenzi wa ufundi

Julai 30, Aston Villa ilitangaza kumuajiri mkurugenzi mpya wa ufundi, Johan Lange kutoka FC Copenhagen ya Denmark kuchukua nafasi ya Jesus Garcia Pitarch ambaye aliachana na klabu hiyo siku moja baada ya kunusurika kushuka daraja. Garcia alitumia kitita cha zaidi ya Pauni 100 milioni (Sh294 bilioni) kufanya usajili wa wachezaji ambao wengi wao walishindwa kuonyesha mchango mkubwa kikosini kama vile Samatta, kipa Pepe Reina na kiungo Danny Drinkwater.

Kuondoka kwa Garcia na ujio Lange kulimaanisha maisha ya wachezaji aliowasajili yalikuwa kikaangoni na haikushangaza kuona Villa ikishindwa kumsajili moja kwa moja Reina aliyekuwa kwa mkopo kutokea Napoli.

Mfumo & mbinu

Akiwa Genk, Samatta aling’ara kwa sababu timu ilijengwa na kucheza kwa kumzunguka yeye, hivyo alijikuta akipata huduma stahiki kutoka kwa viungo na wachezaji wengine wa timu hiyo.

Hata hivyo ndani ya Aston Villa, hakukutana na hali hiyo kwani timu ilicheza kwa kumtegemea nahodha Jack Grealish na hivyo kumfanya Samatta akose huduma za mara kwa mara ndani ya eneo la hatari la Villa, jambo lililomuweka katika wakati mgumu.

Mchambuzi Azam afunguka

Mchambuzi wa soka wa kituo cha Azam TV, Ally Kamwe anasema mabadiliko ya mkurugenzi wa ufundi yamemwangusha Samatta pamoja na presha ya timu. “Kwanza kabisa kitendo cha Aston Villa kumuajiri Johan Lange kuwa mkurugenzi wa michezo mpya kilikuwa na ishara mbaya kwa Samatta kwa sababu huyu alikuja na mpango mpya uliohitaji wachezaji wapya anaowaamini. Samatta hakuwa kwenye orodha hiyo

Pili Samatta aliingia Villa ikiwa na presha kubwa sana. Ilikuwa changamoto kubwa kwake kuzoeana na wenzake/mazingira ya Ligi. Timu ikiwa na presha ya kushuka daraja,” alisema Kamwe.