Mama Bocco...Simba ilipo yupo

SHABIKI wa Simba, Rehema Kamburuta 'Mama Bocco' amesema kwa msimu huu tangu uanze amekosa mechi mbili za mikoani dhidi ya Polisi Tanzania (Moshi) na Prisons (Sokoine).

Mama huyo mwenye watoto wanne ambao ni Idrissa (32), Pili (29), Mohamed (25) na Mwansada (10), amesema nauli za kusafiri kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania analipiwa na watoto wake.

"Wanangu wamekuwa wakubwa, hawawezi kunishangaa kwa nini nazunguka kila mkoa kuishangilia Simba wanajua ninavyoipenda na kupata shida, uzuri na wao ni Simba damu;

Ameongeza "Kama sijaonekana uwanjani basi nakuwa nimepatwa na shida kubwa inayonifanya nishindwe kabisa kwenda Simba inapocheza."

Mama huyo mwenye umri wa miaka 54 amesema amejipachika jina la mama Bocco kwa sababu ya nidhamu ya kazi aliyonayo nahodha wa timu hiyo.

"Bocco anajua kwamba namkubali sana, namchukulia kama mwanangu, maana Nina watoto wakubwa ana heshima na anawajibika ipasavyo uwanjani,"amesema.

Pia amewata wacheza ambao hapendi wakosekane kikosi cha kwanza kuwa ni Aishi Manula, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shomari Kapombe,  Joash Onyango, Henock Inonga, Jonas Mkude, Clatous Chama, Sakho, Kibu Denis, Moses Phiri na  John Bocco.

"Wachezaji hao nikiwaona najisikia burudani kabisa, ingawa siwezi kuingilia kazi ya kocha mkuu, Juma Mgunda ndiye anawajua zaidi wachezaji wake," amesema.