Makocha wapya Simba kuwahi kambi Jumatatu

Kikosi cha Simba kinatarajia kuanza mazoezi Jumatatu mara baada ya mapumziko zaidi ya wiki moja ambayo walipewa wachezaji na benchi la ufundi baada ya kutoka katika kombe la Mapinduzi na uongozi unatarajia kumtangaza kocha mpya mapema.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kikosi hicho kitaanza mazoezi Jumatatu, muda wanaoamini watakuwa wameshamalizana na makocha wapya wawili.

Try Again alisema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa Kocha Kuu ambaye ataingia nchini wakati wowote kuanzia sasa na Jumatatu ijayo atakuwa katika uwanja wao wa mazoezi Mo Bunju Arena akiwanoa wachezaji wa kikosi hicho.

“Mchakato wa kutafuta kocha hakuwa mrahisi kwetu kwani, ila tumefanya mchujo mpaka kumpata mmoja ambaye mara baada ya kumtambulisha ataanza majukumu ya kukinoa kikosi chetu Jumatatu katika maandalizi ya Ligi ya mabingwa Afrika, Ligi Kuu Bara na mashindano mengine,” alisema Try Again ambaye alikataa kuliweka jina hadharani hata alipoombwa.

“Siwezi kumtaja jina lake wakati huu kwani tupo katika hatua za mwisho kumalizana nae na baada ya hapo ndio kila kitu kitakuwa wazi mara baada ya kukamilisha taratibu na mchakato mingine yote ya kumpata,” alisema na kuongeza;

“Habari njema zaidi kwetu tupo pia katika hatua za mwisho kumalizana na kocha mpya wa makipa ambaye nae mara baada ya kuja nchini na kumaliza nae tutamtangaza na ataanza majukumu yake mara moja kama ilivyokuwa kwa huyo mkuu wa benchi la ufundi.

“Kocha wa makipa nae atakuwa sehemu ya mazoezi katika kikosi chetu ambacho kitaanza maandalizi yake Jumatatu kwa wachezaji wote waliokuwa hawapo katika majukumu ya timu zo za taifa,” alisema Try Again.

“Kuhusu wachezaji wapya ambao tutawatumua katika Ligi ya mabingwa Afrika bado tunaendelea na mchakato wa kutafuta wale ambao tunawahitaji kulingana na mapungufu yetu ili kwenda kufanya vizuri kwenye mshindano haya makubwa,” aliongezea Try Again.

Miongoni mwa makocha wanaotajwa kuomba kazi na Simba walikuwa karibu nao ni wa Afrika Kusini wawili, Eric Tinkle ambaye ni kocha wa zamani wa Maritzburg United, Clinton Larsen ambaye alifundisha Polokwane City zote za Ligi Kuu nchini humo na Malgeria Adel Amrouche ambaye kwa sasa anafundisha timu ya taifa ya Botswana.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa, (BMT), Kanali Idd Kipingu alisema Simba inahitaji kupata kocha mwenye uamuzi kwa wachezaji na uongozi.

“Ukiachana na uwezo na ubora wake, lakini awe mkweli, akisema hii ni nyeupe basi iwe hivyo na uongozi umwamini, pia wachezaji wamtii na mwenye uwezo wa kuzungumza na wanachama,” alisema.

Alisema kwa namna ilipofika Simba kisoka inahitaji kuwa na kocha atakayemudu kushusha presha ya uongozi,wanachama na wachezaji, ingawa kikubwa zaidi ametaja kuwa ni uwezo wake, anapaswa kuwa amebobea katika taaluma hiyo.

Simba itaanza kucheza mechi za viporo kuanzia Februari 4 baada ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kutoa taarifa ya ligi itakayoendelea Februari 13 mzunguko wa 19.