Makocha Simba, Yanga watambiana

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Makocha wa Simba na Yanga kila mmoja ametamba kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi ambapo fainali zake zinafanyika kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Wakizungumza leo Jumanne na Waandishi wa Habari, makocha hao walisema ingawa hakuna fainali nyepesi lakini wanahitaji kutwaa ubingwa huo ili kuwapa burudani mashabiki wao

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze amesema mazoezi ya leo jioni ndiyo yatampa mwanga wa kujua ni mchezaji gani atakuwa fiti kuwakabili Simba ingawa akisisitiza kwamba kipa wake Farouk Shikhalo ndiye atakaa langoni.

"Shikhalo nilipanga atumike mechi zote za huku na ndicho kilichotokea hata kesho hakutakuwa na mabadiliko kwenye safu hiyo labda itokee vinginevyo, upande wa wachezaji wa ndani nitaangalia kwa mara ya mwisho kwenye mazoezi ya leo jioni,

"Simba ni timu nzuri na inafanya vizuri hivyo ni lazima tujiandae kwa hilo kwani lengi letu ni ushindi ambao utaamuliwa na dakika 90 kwani kila timu inataka ubingwa," amesema Kaze

Kuhusu Said Ntibankonziza na Yacouba Songne ambaye aliumia jana walipocheza na Azam mechi ya nusu fainali ambapo alishindwa kumalizia mchezo huo, Kaze alifafanua kwamba,

"Saido sitamtumia kwenye mechi ya fainali ila Yacouba nitaangalia baadaye wakati wa mazoezi," amesema Kaze

Kwa upande wa Seleman Matola naye ametamba kutwaa ubingwa huo ingawa amesema anawaheshimu Yanga kwani kadri siku zinavyokwenda kikosi chao kinaimarika.

"Hakuna fainali nyepesi kama alivyosema kocha hapa, kikubwa ni kujiandaa na wachezaji waliopo ndio nitakaowatumia ila itategemea na namna nitakavyowaona kwenye mazoezi ya baadaye.

"Mashindano haya yana ushindani mkubwa, tumefika fainali tukiwa tumejipanga kwani Yanga ni timu nzuri na wameimarika zaidi kwasasa," amesema Matola