Makocha: Simba itarudi kibabe

SIMBA inakiwasha na Biashara leo jioni mjini Musoma. Makocha wamekitazama kikosi hicho na kusema wana imani kubwa kitafanya vizuri kwenye mashindano watakayoshiriki msimu ujao ndani na yale ya kimataifa.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti jana, makocha hao wamesema Simba kufungwa na Yanga na TP Mazembe siyo kigezo cha kuishusha thamani.

Kocha wa zamani wa Biashara United, Amani Josiah alisema; “Nilivyowatazama Simba wako vizuri kiufundi na mchezaji mmojammoja wako vizuri. Kwa jinsi walivyocheza na Yanga, ilikuwa ni mbinu pale walikuwa wanapambana halikuwa suala la vita ya mchezaji mmojammoja. Kuna nyakati mwalimu kile alichokuwa anataka kukifanya hakikufanyiwa kazi huenda kulingana na utimamu wa wachezaji wa upande wake. Wachezaji wa Simba hawakuonyesha ule ufiti wa kushindana.”

Ukiwaangalia uwezo wa mchezaji mmojammoja kuanzia ulinzi kuja kiungo na ushambuliaji, wana watu wa kumaliza mechi, wa kucheza mpira, kumiliki mchezo na wenye maamuzi yanayohitajika katika kila eneo. Kilichopungua ni kukosa ule uharaka wa mechi ambao hauwezi kuja siku ya kwanza,” alisema Josiah.

“Mwalimu anaonekana yuko vizuri. Ana mipango A na B ambayo yote ilikuwa vizuri lakinini wachezaji tu kutokuwa fiti ndio kuliwafanya wasipate kile walichokitegemea juzi ila wakifanyia kazi watafika mbali,” alisema Josiah.

Mwenyekiti wa Chama cha Makocha mkoa wa Mwanza, Kessy Mziray, alisema; “Usajili wa Simba una malengo ya sasa na baadaye pili ni jukumu sasa la kocha kutengeneza mfumo utakaoendana na wachezaji waliopo kwa sasa na mwisho anachotakiwa kufanya kocha ni kupata wachezaji watakaofiti kwenye kila idara hasa kwenye kiungo na ushambuliaji”